NHIF YATOA MIFUKO 245 YA SARUJI KUSAIDIA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA YA MUHEZA

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya nchini (NHIF)umekabidhi mifuko 245 ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Muheza inayojengwa eneo la Lusanga ambayo itaondoa changamoto ambazo walikuwa wakikumbana nazo wananchi.

Makabidhiano hayo yalifanyika juzi wilayani Muheza na Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Tanga Ally Mwakababu kwa Mkuu wa wilaya hiyo Mhandisi Mwanasha Tumbo ambapo mifuko hiyo itasaidia ujenzi huo

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo wa saruji,Mkuu wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha aliushukuru mfuko huo kwa kuona umuhimu kusaidia juhudi walizoanzishwa za ujenzi wa hospitali hiyo ili kuwapunguzia adha wananchi ikiwemo kuunga mkono jitihada za harambee iliyoendshwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu.

Alisema msaada huo umefika wakati muafaka wakiwa kwenye harakati za kuendelea na ujenzi wa hospitali hiyo ambao ni muhimu kwa ustawi wa wakazi wa wilaya hiyo katika kuhakikisha wanakuwa nayo ili iweze kuwahudumia.

Mkuu huyo wa wilaya alisema ujenzi wa hospitali hiyo ambao utagharimu bilioni 11 mpaka itakapo kamilika lakini hatua iliyopo kwa harambee walioifanya Jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu waliweze kupata bilioni 1.7.

Alisema na michango mingine tayari walikwisha kukusanya milioni 100 zinawawezesha kuendelea na ujenzi ambapo fedha hizo zilizokusanywa sambamba na vifaa pamoja na ahadi zitakawawezesha kukamilisha majengo mawili ya ikiwamo wodi za wazazi na watoto ambao tayari wameanza ujenzi wake unaendelea.

“Lakini wapo ambao walitoa vifaa mbalimbali ikiwemo Milango,Saruji,Matofali na Mabati jambo ambalo limetupa nguvu kubwa kuendelea na shughuli za ujenzi kwa lengo la kuhakikisha hospitali hiyo inakamilika na kuweza kuwahudumia wananchi “Alisema DC Mwanasha.

Aidha alisema wanaishukuuru pia serikali kwakutupangia bajeti ya mwaka huu ya fedha kiasi cha sh.bilioni 1.5 hivyo tuna uhakika wa kujenga majengo maengine na kuwawezesha ujenzi wake kwenda kasi na ubora unaotakiwa.

Hata hivyo alisema katika harambee hiyo ambayo iliongozwa na Makamu wa Rais wapo wadau ambao walihudhuria wamesaidi kusaini nao mkataba wa sh.milioni 100 na wanategemea kuchimba kisima na ujenzi wake utaanza baada ya mvua kupungua.

Naye kwa upande wake Meneja wa Mfuko huo mkoani Tanga Ally Mwakababu akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo alisema wameamua kuchangia ujenzi huo ikiwa ni kama sehemu ya kuunga mkono jitihada zilizoanzishwa.

Alisema wao kama taasisi wapo tayari kuona juhudi zilizoanzishwa kuhakikisha wananchi wanaondokana na changamoto mbalimbali kwenye huduma za afya ili waweze kutekeleza vema majukumu yao ya kila siku ya kujiletee maendeleo.