HATUTAVUMILIA UDANGANYIFU ...

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema hautamvumilia mtoa huduma yoyote atakayejihusisha na udanganyifu katika utoaji wa huduma kwa wanachama na badala yake utamfungia mara moja usajili alionao.

Aidha umewataka kuwaeleza ukweli wanachama juu ya huduma wanazotoa kulingana na ngazi ya kituo husika na sio kutoa visingizio kwa wanachama kuwa baadhi ya huduma hazitolewi ama kulipiwa na Mfuko.

Hayo yalisemwa katika Mkutano wa siku moja uliofanyika Dar es Salaam jana ambao ulikutanisha watoa huduma wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Akijibu hoja mbalimbali, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema kuwa udanganyifu wowote utakaobainika kufanywa na watoa huduma hautavumiliwa kwa namna yoyote na badala yake hatua za kisheria na kufungiwa kituo zitachuliwa.

“Tunapobaini fomu ya mgonjwa imesainiwa na daktari ambaye hakumhudumia kwa kweli niwe wazi kabisa kuwa sitavumilia na lugha rahisi tu huo ni wizi au uhujumu wa Mfuko…NHIF tunaitegemea watanzania wote na sisi ambao tumepewa dhamana lazima tuhakikishe tunaulinda hivyo kama ni kufungia kituo nitafunga,” alisema Bw. Konga.

Alitumia mwanya huo pia kuwaomba watoa huduma kuwaeleza ukweli wanachama wa Mfuko juu ya suala la miongozo ya huduma kulingana na ngazi ya kituo husika na kuacha tabia ya kurusha lawama kwa Mfuko.

“Tuwe wakweli mwanachama anapofika kwako, yawezekana kituo chako kina wataalam wa kutosha na vifaa tiba vya kisasa lakini kulingana na ngazi ya kituo chako huruhusiwi kutoa baadhi ya huduma hivyo msiwadanganye wanachama kuwa huduma hizo hazilipiwi bali waelekezeni mahali pa kuzipata,” alisema.

Alisema kuwa Mfuko unafanya kazi zake kwa kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekewa hivyo kila upande uhakikishe unatimiza wajibu wake ili kuwaondolea usumbufu wanachama lakini pia kuboresha huduma.

Kwa upande wa watoa huduma ambao waliwakilishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dk. Grace Magembe alipongeza kwa hatua kubwa iliyofikiwa na NHIF lakini akatoa rai kwa pande zote mbili kubadilika katika utendaji kazi kwa kuwa wananchi wanahitaji majibu na suluhisho la matatizo yao haraka.

Kwa upande wa Watoa huduma binafsi wanaoongozwa na Taasisi ya Watoa Huduma Binafsi (APHTA) ambao waliwakilishwa na Mwenyekiti wao Dk. Samuel Ogillo ambaye aliungana na kauli ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Konga kuwa kwa upande wao hawatavumilia kuona udanganyifu ukifanywa dhidi ya Mfuko huo.

Mkutano huo ulifunguliwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF, Mama Anne Makinda ambaye aliwataka kutumia lugha yenye staha kwa wagonjwa ili kuondokana na malalamiko yasiyokuwa na msingi