wavuviZAIDI ya vikundi 36 vyenye zaidi ya wanachama 24,000 vimeshaanza kunufaika na huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kupitia Mpango wa KIKOA ambao unalenga makundi ya wajasiriamali nchini.

Hivi Mfuko umekabidhi kadi kwa wanachama wapya ambao ni wanachama wa Umoja wa Wavuvi Wadogo wa Dar es Salaam (UWAWADA), kundi ambalo limehamasisha na huduma za Mfuko kupitia mpango huo.

Akizungumzia hilo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Michael Mhando, Mpango wa KIKOA unawapa nafasi wanachama wa  vikundi husika kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na kunufaika na mafao ya matibabu sawa sawa na wanachama wanaochangia kupitia mishahara yao ya kila mwezi.

“Hadi sasa utaratibu huu umeshaanza kuwanufaisha wanachama wa vikundi zaidi ya 36 vyenye wanachama zaidi ya 24,000. Wanachama wa vikundi hivi wanajishughulisha na shughuli mbalimbali za ujasiriamali chini ya mwamvuli wa Vicoba, Saccos, Amcos, vyama vya madereva wa teksi, bodaboda na kadhalika,” alisema Mhando.

Mhando alisema katika hafla hiyo ya jana kuwa dhamira yao ni ya kuyafikia makundi yote ya wajasiriamali wadogo na wakubwa ili kuwajumuisha katika mpango huo, na kwamba Uwawada ni wadau muhimu, ndio maana umeona utoe mchango wake kwa kuangalia afya zao na kuwaletea mpango huo wa kuchangia kabla ya kuugua ili kuwa na uhakika wa tiba wakati wote hata kama hawana fedha mfukoni.

Ili kunufaika na mpango huo wa KIKOA, mwanachama atatakiwa kuchangia Sh 76,800 kwa mwaka kwa mtu mmoja, mchango ambao utampa fursa ya kupata huduma za matibabu katika vituo vya tiba vilivyosajiliwa na NHIF nchini kote, na mchangiaji anaweza kuongeza mtegemezi wake kwa kuchangia kiasi hicho hicho.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, nia yao ni kuwafikia wavuvi zaidi ya 20,000 katika ukanda wa Bahari ya Hindi kuanzia Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Rufiji, Kilwa, Mafia, Bagamoyo, Pemba na Unguja.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi yake, Mohamed Masoud alisema awali alikuwa anatumia fedha nyingi kwa ajili ya matibabu, lakini kwa kuwa na kadi ya NHIF, hivi karibuni alitibiwa bila malipo, hivyo kuokoa fedha nyingi ambazo angelazimika kuzitoa mfukoni kwake.

Naye Faisal Ally ambaye ni kuwa mwanachama wa bima ya afya ni suluhisho la kudumu la afya zao kwani kutokana na biashara yao yenye kipato kidogo, unapougua hali inakuwa mbaya na wakati mwingine huna fedha wakati huo, hivyo sasa watanufaika na matibabu, huku akiahidi kuwa ndani ya miaka mitano ijayo, wavuvi zaidi ya 20,000 watakuwa wamejiunga na NHIF ambayo ina lengo la kuwafikia Watanzania wote.