Waziri Mkuu

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda  ameuagiza uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuongeza wigo wa utoaji wa elimu kwa jamii ya namna ya kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na magonjwa ambayo yanaleta unyanyapaa ndani ya jamii.

Mbali na hilo pia Waziri Mkuu amekiri kuridhishwa na jitihada za makusudi zinazofanywa na Mfuko huo ambazo zimesababisha mpaka sasa kuhudumia jumla ya asilimia 23 ya watanzania wote.

Hayo aliyasema hivi karibuni mkoani Lindi wakati akitembelea Taasisi mbalimbali zilizoshiriki kwenye maonesho ya Kitaifa ya Nane Nane  katika viwanja vya Ngongo.

“Kazi mnayofanya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ni nzuri mno, idadi ya Watanzania ambao mmeweza kuwafikia ni kubwa ikiwemo na mipango mliyonieleza hapa ya kuendelea kuongeza wigo wa wanachama… kwa upande wa elimu hasa hii mnayoitoa ya namna ya kuishi mtindo bora wa maisha na kuepukana na magonjwa ya kuambukiza mnafanya vizuri ila angalieni sasa na haya magonjwa mengine ambayo yanawafanya watu wanyanyapaliwe na jamii,” alisema Pinda.

Alisisitiza kuwa kutoa elimu juu ya magonjwa hayo yakiwemo ya ngozi itaisaidia jamii kwa kiwango kikubwa kuishi na kuwahudumia wagonjwa hawa kwa upendo na kuachana na unyanyapaa unaofanywa kwa baadhi ya wanajamii.

Waziri Mkuu Pinda alipata fursa ya kukagua huduma zote za Mfuko ambazo zinatolewa katika maonesho hayo ambazo ni pamoja na elimu kwa umma inayohusiana na huduma zinazotolewa, namna ya kujiunga na faida za mwanachama wa Mfuko. Huduma zingine ni upimaji wa saratani ya matiti, shinikizo la damu na kiwango cha sukari.

Awali Waziri Mkuu alipokea maelezo ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko kutoka kwa Mkurugenzi wa Masoko na Utafiri Bw. Rehani Athumani ambaye alisema kuwa, Mfuko umejikita katika kuhamasisha Watanzania wajiunge na huduma zake ili wawe na uhakika wa kupata matibabu wakati wote.

Bw. Rehani alisema kuwa, Mfuko umeangalia makundi yote na kuweka taratibu ambazo zitawawezesha wananchi kila mmoja kwa nafasi yake kuweza kunufaika na huduma za Mfuko. “Kwa sasa Mfuko unao mpango wa KIKOA ambao unawawezesha wajasiliamali kujiunga na Mfuko kwa gharama ndogo hivyo tunaamini kabisa wananchi wote watanufaika,” alisema Bw. Rehani.

Alisema kuwa kwa sasa Mfuko umesogeza huduma zake kwa wananchi kwa kuwa na ofisi kila Mkoa ambapo elimu ya afya inawafikia zaidi wananchi katika maeneo yote ya mijini na vijijini.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mwantumu Mahiza alisema kuwa katika uongozi wake mkoani hapa atahakikisha asilimia kubwa ya wananchi wanajiunga na huduma za Mfuko ikiwemo na Mfuko wa Afya ya Jamii ili wananchi wa Lindi wawe na uhakika na matibabu.