Rais Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Jakaya Kikwete na mke wake Mama Salma Kikwete wanatarajia kuanza rasmi kutumia huduma za matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Rais Kikwete na mkewe amekabidhiwa kadi za matibabu hivi karibuni wakati akiwa mkoani Tanga katika hafla ya maalumu ya kuagana na wananchi wa mkoa huo.

Akipokea kadi hizo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mfuko wa Afya ya Jamii Eugen Mikongoti ambaye alimwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Michael Mhando, Rais Kikwete alionesha kufurahishwa kwa kupata kadi hiyo ya matibabu kwani sasa ana uhakika kuwa yeye na mkewe watapata matibabu katika hospitali yoyote nchini kwa kutumia kadi hizo.

Aidha amewahimiza wananchi wengine kujiunga na Mfuko huo kupitia taratibu mbalimbali ili kuondokana na unyonge wa kuhangaika kutafauta fedha za matibabu wanapougua.

Amesema utaratibu wa kuchangia bima ya afya kabla ya kuugua unawapa wananchi utulivu wa akili kwani wanakuwa na uhakika wa kutibiwa hata kama hawana fedha Mfukoni.

Rais Kikwete amewahimiza watendaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuendelea kutoa elimu umma kuhusu umuhimu wa kujiunga na Mfuko huo ili kufikia lengo la afya bora kwa wote ifikapo mwaka 2025.

Kwa upande wa NHIF, Bw. Mikongoti amemwambia Rais kuwa hadi kufikia mwezi Juni 2015, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulikuwa unahudumia asilimia 23.1 ya Watanzania wote Milioni 44 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.

Amesema ana imani kuwa lengo hilo litafikiwa kutokana na mikakati inayotekelezwa na Mfuko huo ikiwa ni pamoja na kusajili makundi mbalimbali ya watanzania wakiwemo wajasiliamali waliomo katika vikundi vilivyosajiliwa katika mpango unaojulikana kama KIKOA.