Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Seif RashidSERIKALI imesema itahakikisha inaongeza idadi ya Watanzania wanaojiunga na mifuko ya afya ambayo ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii ili wawe na uhakika wa kupata matibabu, lakini pia uboreshaji wa huduma
za afya.

Jitihada za kuongeza idadi hiyo zimeahidiwa katika hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Rashid Seif ambayo aliiwasilisha katika kikao cha Bunge cha Bajeti Juni 2, mwaka huu mjini Dodoma.

Katika hotuba yake, Dk. Seif alisema kuwa moja ya vipaumbele vya Wizara katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 ni kuhamasisha wananchi ili wajiunge na mfumo wa bima ya afya.

“Sera ya Afya ya mwaka 2007 inaelekeza kuwa wananchi wote wapate huduma za afya bila kikwazo cha fedha wala kujali hali yao ya kiuchumi katika jamii,” alisisitiza.
Katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 ilidhamiria kufikia asilimia 30 ya Watanzania wote waliojiunga kwenye mifuko ya afya ambapo mpaka kufikia Machi 2015 ni asilimia 22.82 ya wananchi wanaofaidika na huduma za mifuko hii.

“Ili kuhakikisha mafanikio haya yanaendelezwa na kuboreshwa, Wizara imeandaa Mkakati wa Ugharamiaji Huduma za Afya nchini unaoainisha njia madhubuti za kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata hifadhi ya jamii katika eneo la afya. Utekelezaji wa mkakati huo utaanza baada kuridhiwa na Serikali kwa mujibu wa utaratibu,” alisema Dk. Rashid.

Akizungumzia mafanikio yaliyofikiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii kwa kuhudumia wanufaika ambao ni asilimia 23, alisema yametokana na juhudi mbalimbali zikiwemo mabadiliko ya sheria ambayo yameuwezesha Mfuko kuongeza uandikishaji wa makundi mbalimbali kama vikundi vya wajasiriamali na ushirika, wanafunzi, Taasisi za kidini, madiwani na mashirika binafsi ambayo awali yalikuwa hayaruhusiwi.

Kwa upande wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bw. Michael Mhando anasema kuwa, Mfuko umejiwekea mikakati ya kuhakikisha idadi kubwa zaidi ya Watanzania wanajiunga ama wanakuwa ndani ya utaratibu wa Bima ya afya.

Anasema kuwa elimu kuhusu umuhimu wa bima ya afya itatolewa katika mikoa yote na itasambazwa kwa njia mbalimbali zikiwemo za vyombo vya habari, vipeperushi na kuwafikia wananchi katika maeneo yao.

Hata hivyo, uboreshaji wa huduma za matibabu unafanyika kila mara ili kuhakikisha wananchi wanavutika zaidi na huduma zake. Kutokana na haya, anawataka wananchi kujiunga na huduma hizi ili wawe na uhakika wa matibabu, lakini pia kufikia lengo la afya bora kwa wote.