NHIF DGDHANA ya afya bora kwa wote ni dhamira na utekelezaji wa hatua za makusudi za kuwakinga wananchi wengi dhidi ya gharama za matibabu kupitia utaratibu wa kisheria zinazowahakikishia wigo wa huduma za matibabu za kinga, kuhamasisha afya, tiba na utengamano.

Nchi nyingi zinaweza kufikia lengo la afya kwa wote kwa njia kuu mbili; ya kwanza ni kupitia mfumo wa kodi ambapo chanzo kikuu cha kugharamia huduma za afya kinatokana na kodi.

Utaratibu huu unatumika katika nchi za Uingereza, nchi za Scandinavia, Ghana na Botswana. Mafanikio ya mfumo huu yanategemea uchumi wa nchi husika, uwezo wa kukusanya kodi, ubora wa mfumo wa kodi na utashi wa kisiasa. Changamoto zake kubwa ni pamoja na muda mrefu wa kusubiri kupata huduma, uduni wa huduma na wigo finyu wa kitita cha mafao.

Kwa nchi za kiafrika changamoto kubwa ni uendelevu wa mfumo, utegemezi na mzigo mkubwa wa fedha kwa Serikali na walipa kodi. Mfumo wa pili ni wa uchangiaji gharama za huduma za afya ambapo chanzo kikubwa ni michango ya wananchi, waajiri na Serikali.

Mfano, Tanzania, Rwanda, Ujerumani,Ufilipino, Japani, Korea Kusini na Nigeria. Faida za mfumo huu ni pamoja na mshikamano,ushirikishwaji wa wadau katika uendeshaji,uendelevu na kupunguza mzigo wa Serikali kugharamia huduma za afya hususan kwa nchi zinazoendelea.

Changamoto za mfumo huu ni utekelezaji wa matakwa ya sheria hasa uchangiaji kwa watu walio katika sekta isiyo rasmi, uwekaji wa viwango vinavyoshabihiana na uwezo wa kuchangia. Aidha, hakuna nchi yoyote iliyofanikiwa kufikia lengo la afya kwa wote kupitia uchangiaji wa hiari. Nchi za Rwanda, Ghana, Ufilipino, Vietnam, Thailand na Korea Kusini ni mifano ya nchi zilizofanikiwa kufikia afya kwa wote kwa kufanya bima ya afya ni lazima kwa kila mwenye uwezo wa kuchangia.

Vilevile, Serikali za nchi hizi zina utaratibu wa kuchangia huduma za matibabu kwa wasio na uwezo wa kuchangia na makundi maalumu. Nchi mbalimbali duniani zinafanya jitihada kubwa kuhakikisha wananchi wao wanapata huduma bora za afya. Yapo pia malengo ya kikanda kama Azimio la Kigali la Afya kwa Wote kupitia Bima ya Afya (2012) kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Utekelezaji wake
Dhana ya Bima ya Afya inatekelezwa kwa kiasi na kiwango kikubwa kupitia utekelezaji wa Sera ya Mabadiliko katika Sekta ya Afya (1993) inayosimamiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Sera hii ndio iliyoanzisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambayo kwa pamoja inahudumia asilimia 97 ya wananchi wote wanaohudumiwa kupitia mifuko ya uchangiaji. Wananchi wanaohudumiwa na mifuko hii miwili ni milioni 9.9 ambayo ni sawa na asilimia 23 ya Watanzania wote, idadi ambayo bado ni ndogo.

Changamoto zilizopo
Changamoto kubwa ni kukosekana kwa mkakati wa kitaifa wa kugharamia huduma za matibabu. Suala la Afya kwa Wote kutoonekana wazi kikatiba kuwa haki ya kibinadamu na uhiari wa kuchangia huduma za matibabu hasa kwa Mfuko wa Afya ya Jamii pamoja na uduni wa huduma za matibabu.

Nchi zilizofanikiwa kufikia lengo la Afya kwa Wote zimeweka kwenye Katiba zao suala hili kama haki ya kibinadamu. Utashi wa kisiasa pia ni muhimu zaidi katika kufikia Afya kwa Wote.

Uzoefu katika nchi nyingi unaonesha kuwa ili kuwafikia wananchi wote zinahitajika jitihada za kuunganisha nguvu za vyanzo mbalimbali vya rasilimali ili kutoa huduma endelevu ikiwemo mfumo wa kodi, michango ya wananchi na Taasisi za Umma na Binafsi zilizopo.

Uzoefu kutoka nchi nyingine
Uzoefu kutoka nchi mbalimbali zilizofikia afya kwa wote au zilizopiga hatua kama Rwanda, Ghana, Thailand, Ufilipino na Korea Kusini,vitasaidia sana nchi yetu kuona namna bora yakufikia lengo hili ambalo kwa sasa ni ajenda ya dunia.