jakaya

RAIS Jakaya Kikwete ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa hatua nzuri ya kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha Uchunguzi wa Magojwa cha Benjamin Mkapa ambacho amekizindua rasmi Oktoba 13, mwaka huu.

 “Nimefurahishwa na hatua hii iliyofikiwa. Kituo hiki ni kikubwa na cha  kisasa na hospitali itakapokamilika itakuwa na vitanda 300, wakati ile inayojengwa Mlonganzila (Dar es Salaam), itachukua vitanda 600, kwa hiyo hii ni kubwa pia. “Hivyo, naushuruku uongozi wa NHIF, Udom na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kusimamia mradi huu vizuri. Hii itakuwa hospitali ya daraja la juu najivunia kukamilika kwa awamu hii,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alionesha furaha yake hiyo wakati wa uzinduzi wa kituo hicho ambapo mbali na yeye kuzindua pia Rais Mstaafu Benjamin Mkapa naye alikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria uzinduzi huo.

Hakusita kutoa pongezi zake za dhati kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emmanuel Humba ambaye ndiye alikwenda na wazo na kujenga kituo hicho Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na Rais kumpa maagizo ya kuanza ujenzi Chuo Kikuu cha Dodoma ambako kulikuwa na eneo kubwa.

Kituo hicho kitajikita zaidi katika magonjwa ya figo ambapo huduma zitakuwa za kusafisha damu na mpaka kubadili figo pamoja na magonjwa ya moyo.

Akitoa maelezo kwa Rais Kikwete, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Shaaban Mlacha, alisema awamu ya kwanza imekamilika, ikiwamo ununuzi wa samani na sasa wanasubiri vifaa tiba na awamu ya pili itakamilika muda mfupi ujao, na kwamba gharama ya ujenzi ni Shilingi bilioni 170.

Alisema tangu Oktoba 9 mwaka huu, hospitali ilianza kutoa huduma kwa wagonjwa zaidi ya 200 wakati ikisubiriwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ijiweke sawa kuendesha hospitali hiyo.

Profesa Mlacha alisema: “Malengo ni kuwa hospitali ya kisasa na bora kuliko zote Afrika Mashariki na ya Kati kama ilivyo Chuo Kikuu cha Dodoma na katika huduma za afya kupitia kituo hicho Tanzania itakuwa ni nchi ya tatu Afrika baada ya Afrika Kusini na Morocco. Alisema kuwapo kwa hospitali maalumu kwa ajili ya matatizo ya figo, tafsiri yake ni kwamba upelekaji wa wagonjwa nje ya Tanzania kwa matibabu utafikia kikomo.