Taasisi ya Kimataifa ya Bima ya Afya Nchini Korea (KOFIH) imepongeza jitihada mbalimbali zilizofanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) za kuhakikisha wanachama wake wanapata huduma nzuri za matibabu lakini pia uboreshaji wa sekta ya afya kwa ujumla.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la KOFIH, Dk.Chang Bae Chug Bae wakati akibadilishana uzoefu na watendaji wa NHIF katika kikao kazi kilichofanyika Ofisi za NHIF Makao Makuu ambapo jumla ya watendaji 28 kutoka nchi za Korea, Ethiopia na Ghana walipotembelea Mfuko huo siku ya tarehe 12 na 12/11/2015.

Katika ziara hiyo ya kikazo ambayo ilikuwa ni ya siku mbili, mada mbali mbali ziliwasilishwa ikiwa ni pamoja na kutembelea ofisi ya Mkoa ya NHIF Mkoa wa Ilala, Kituo cha kutolea huduma cha Mnazi Mmoja, Kituo cha kutunza kumbukumbu za wanachama na Kituo cha kisasa cha kuhifadhia kumbukumbu zote za Mfuko huo.

“Tumekuja Tanzania kwa lengo la kujifunza namna ya utoaji na uendeshaji wa huduma unaofanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya lakini pia kubadilishana uzoefu wetu na wao kwa lengo la kuboresha zaidi huduma zetu kwa wananchi ndani ya nchi zetu...lakini tumeona wenzetu wamefanya jihudi kubwa sana ambazo ni za kupigiwa mfano,” alisema Dk.Chang.

Awali akiwakaribisha wageni hao Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Michael Mhando alisema kuwa Mfuko kupokea wataalam wa masuala ya afya kutoka nchi hizo ni sifa kwa nchi kutokana na uendeshaji mzuri wa Mfuko huo ambao nchi zingine zinakuja kujifunza.

“Ni heshima ya pekee kwetu NHIF kupokea ugeni mkubwa kama huu ambao nao wameona kazi kubwa tuliyofanya ukilinganisha na nchi zingine hivyo imetupa fursa ya sisi kujifunza zaidi namna wenzetu wanavyofanya kwa kubadilishana mawazo ya kikazi,” alisema Bw. Mhando.

Alisema kuwa jitihada za Serikali kupitia Mfuko ni kuwaunganisha Watanzania wote na mfumo wa Bima ya Afya ili kila mmoja awe na uhakika wa kupata huduma za matibabu.

Aidha alitumia mwanya huo kusisitiza kuwa NHIF itaendelea na jitihada za uboreshaji wa sekta ya afya kupitia utoaji wa mikopo ya vifaa tiba, ukarabati wa majengo na ujenzi wa vituo vya kisasa vya utoaji wa huduma za matibabu na uchunguzi wa magonjwa.