Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya jana uliungana na Watanzania wote katika kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli kwa kufanya usafi katika maeneo yote ya ofisi za Mfuko.

Mbali na kufanya usafi katika mazingira yanayozunguka ofisi zake, Mfuko ulitumia fursa hiyo kutembelea Hospitali ya Jeshi la Polisi iliyoko Barabara ya Kilwa.

Akiongoza watumishi wa Mfuko katika maadhimisho hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko, Michael Mhando alisema kuwa zoezi la usafi litakuwa endelevu kwa kuwa mbali na mambo mengine litasaidia katika kuondokana na magonjwa kama kipindupindu na Malaria.

“Sisi kama Mfuko hili tamko la Rais tunaliunga mkono na tutaendelea kulitekeleza muda wote kwani zipo faida kubwa katika kuyafanya mazingira kuwa safi...itatusaidia sana Mfuko kupunguza hata gharama za matibabu kwa magonjwa yanayosababishwa na uchafu wa mazingira,” alisema.

Mfuko pia ulitumia fursa hiyo kutembelea hospitali ya Jeshi la Polisi Kilwa Road ambapo msaada wa mashuka 100 ulikabidhiwa kwa ajili ya kuhudumia wanachama na wananchi kwa ujumla.