Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Michael Mhando akimsalimia mmoja wa wagonjwa ambaye tayari

alikuwa kwa Daktari Bingwa wa njia za mkojo na vibofu.

Sehemu ya wagonjwa wakisubiri kuelezwa utaratibu wa kuwaona madaktari bingwa waliofika hospitalini hapo.

Na Mwandishi Wetu, Kagera

WANANCHI mkoani Kagera wametakiwa kutumia fursa iliyotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ya kupeleka Madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali katika Hospitali ya Mkoa huo kwa muda wa siku saba.

Madaktari hao wametoka katika Hospitali mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Mifupa (MOI), Hospitali ya Rufaa Bugando, Hospitali ya Ndolage na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambao watatoa huduma kwa wanachama wa Mfuko na wananchi wote ambao wana mahitaji ya huduma za kibingwa.

Akitoa mwito huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Michael Mhando alisema kuwa Mfuko ulifikia uamuzi huu kutokana na ukweli kwamba wanachama wote wa Mfuko wanatakiwa kupata huduma sawa katika maeneo yote.

“Wanachama wetu wanatakiwa kupata huduma sawa katika maeneo yote hivyo walioko Dar es Salaam na walioko Mwanza wapate huduma sawa na walioko Kigoma ama Kagera hivyo tukaona kuna umuhimu wa kusogeza hizi huduma ili kuwapunguzia usumbufu wanachama na wananchi kwa ujumla,” alisema Bw. Mhando.

Alisema kuwa ujio wa wataalam hao katika hospitali hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya hospitali hiyo lakini pia watumishi watanufaika na utaalam wa madaktari hao.

“Hii ni fursa ya pekee niwaombe kabisa muitumie ipasavyo, sisi Mfuko kazi yetu ni kuhakikisha tunawasogezea huduma na kuboresha katika maeneo ya vituo vyetu ili wanachama wetu wapate huduma kwa heshima inayotakiwa hivyo mbali na watalaam hawa tumeleta vifaa tiba, dawa na mashuka ili yatumike hapa,” alisema Bw. Mhando.

Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Nasoro Mlambila alisema kuwa ujio wa wataalam hao ni faraja kubwa kwa Mkoa huo kutokana na ukweli kwamba una uhaba mkubwa wa madaktari bingwa hali inayosababisha wananchi kupata shida kubwa.

“Tunao madaktari watatu tu hapa na mahitaji ni makubwa sana hivyo ujio wa wataalam wa masuala ya watoto, wanawake, moyo, njia ya mkojo na vibofu ni msaada mkubwa sana kwa wana Kagera hivyo niwashukuru sana Mfuko kwa jitihada hii kubwa ambayo mmeifanya,” alisema.

Katika hatua nyingine Mfuko ulisema kuwa hautawavumilia watumishi katika hospitali hiyo wanaojihusisha na vitendo vya kughushi nyaraka za kuchukulia dawa katika maduka ya dawa na kuusababishia Mfuko kulipa fedha ambazo hazijatumika kihalali.

“Niseme tu kwamba tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali zikiwemo za kuwaonya kwa barua na wengine kuwafutia usajili na wengine kuwafikisha mahakamani watoa huduma ambao wanajihusisha na vitendo vya udanganyifu lakini niseme kwamba kwa hospitali hii natangaza rasmi kuwa kuanzia sasa naanza kuchukua hatua kali kwa watumishi ambao watabainika kujihusisha na udanganyifu wowote,”,” alisema Bw. Mhando.

Alisema kuwa Mfuko unalo jukumu la kulinda fedha za wanachama wake na kuhakikisha zinatumika katika matumizi sahihi hivyo hauko tayari kuendelea kuvumilia watoa huduma ambao sio waaminifu.

“Nawaomba sana toeni huduma kwa wanachama wetu na sio kutumia vitambulisho vyao kughushi nyaraka mbalimbali zikiwemo za kuchukulia dawa katika maduka ya dawa…sisi tuko tayari kusaidia kituo chochote katika uboreshaji wa huduma zake ili wananchi wanufaike kwa ujumla na sio kikundi cha watu wachache,” alisema Bw. Mhando.

Aidha amewataka kuangalia namna ya uboreshaji wa huduma zake hususan upatikanaji wa dawa ambao umeonekana kuwa tatizo kubwa linaloikosesha mapato hospitali hiyo.

Alisema kuwa mpaka sasa Hospitali ya Mkoa wa Kagera imekuwa ikipoteza mapato mengi kutokana na ukosefu wa dawa na vipimo ambavyo ndivyo vinaingiza fedha nyingi katika vituo vya kutolea huduma hali ambayo inakwamisha uboreshaji wa huduma.

“Mapato mnayopata kwa kweli niseme kwamba hayalingani na ukubwa ama huduma mnazopaswa kuzitoa na hii inasababishwa na ukosefu wa dawa na huduma zingine hivyo hakikisheni mnaboresha haya maeneo ….Mfuko uko tayari kushirikiana na nyie ili kuifanya hospitali iwe na huduma nzuri kwa ajili ya Watanzania…mapato kidogo yanawanyima fursa ya kunufaika na mikopo yetu hivyo naomba hili eneo mlifanyie kazi kwa maslahi yetu sote,” alisema Bw. Mhando.

Mwisho.