Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Michael Mhando akikabidhi msaada uliotolewa na Mfuko kusaidia zoezi

la huduma za Madaktari Bingwa. Msaada huo ni pamoja na vifaa tiba, dawa na mashuka 300.

Na Grace Michael, Kagera

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya umesema hautawavumilia watumishi katika hospitali ya Mkoa wa Kagera wanaojihusisha na vitendo vya kughushi nyaraka za kuchukulia dawa katika maduka ya dawa na kuusababishia Mfuko kulipa fedha ambazo hazijatumika kihalali.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Bw. Michael Mhando ameyasema hayo mjini hapa wakati akizungumza na uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Kagera kabla ya uzinduzi wa mpango wa Madaktari Bingwa ambao wamepelekwa na Mfuko huo kutoa huduma kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.

“Niseme tu kwamba tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali zikiwemo za kuwaonya kwa barua na wengine kuwafutia usajili na wengine kuwafikisha mahakamani watoa huduma ambao wanajihusisha na vitendo vya udanganyifu lakini niseme kwamba kwa hospitali hii natangaza rasmi kuwa kuanzia sasa naanza kuchukua hatua kali kwa watumishi ambao watabainika kujihusisha na udanganyifu wowote,”,” alisema Bw. Mhando.

Alisema kuwa Mfuko unalo jukumu la kulinda fedha za wanachama wake na kuhakikisha zinatumika katika matumizi sahihi hivyo hauko tayari kuendelea kuvumilia watoa huduma ambao sio waaminifu.

“Nawaomba sana toeni huduma kwa wanachama wetu na sio kutumia vitambulisho vyao kughushi nyaraka mbalimbali zikiwemo za kuchukulia dawa katika maduka ya dawa…sisi tuko tayari kusaidia kituo chochote katika uboreshaji wa huduma zake ili wananchi wanufaike kwa ujumla na sio kikundi cha watu wachache,” alisema Bw. Mhando.

Katika hatua nyingine aliitaka Hospitali hiyo kuangalia namna ya uboreshaji wa huduma zake hususan upatikanaji wa dawa ambao umeonekana kuwa tatizo kubwa linaloikosesha mapato hospitali hiyo.

Alisema kuwa mpaka sasa Hospitali ya Mkoa wa Kagera imekuwa ikipoteza mapato mengi kutokana na ukosefu wa dawa na vipimo ambavyo ndivyo vinaingiza fedha nyingi katika vituo vya kutolea huduma hali ambayo inakwamisha uboreshaji wa huduma.

“Mapato mnayopata kwa kweli niseme kwamba hayalingani na ukubwa ama huduma mnazopaswa kuzitoa nah ii inasababishwa na ukosefu wa dawa na huduma zingine hivyo hakikisheni mnaboresha haya maeneo ….Mfuko uko tayari kushirikiana na nyie ili kuifanya hospitali iwe na huduma nzuri kwa ajili ya Watanzania…mapato kidogo yanawanyima fursa ya kunufaika na mikopo yetu hivyo naomba hili eneo mlifanyie kazi kwa maslahi yetu sote,” alisema Bw. Mhando.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dr. Thomas Rutachunzibwa aliunga mkono kuchukuliwa kwa hatua zozote kwa wanaojihusisha na udanganyifu ili kuleta nidhamu ya kazi katika maeneo yao.

Alitumia fursa hiyo kuupongeza Mfuko kwa jitihada mbalimbali ambazo imekuwa ikifanya katika kusogeza huduma kwa wateja ikiwemo ya kupeleka madaktari bingwa katika hospitali hiyo.

“Kitendo cha kutuletea wataalam hapa kwanza kitasaidia kuongeza mapato yetu lakini pia utaalam utakaoachwa kwa watumishi wetu hapa utaendelea kutumika hivyo tunawashukuru sana,” alisema.

Mwisho.