Madaktari bingwa kunufaisha maeneo yote.

Na Mwandishi Wetu, Ruvuma

SERIKALI imesema kuwa itapanga mgawanyo maalumu wa Madaktari na Madaktari Bingwa ili mikoa yote iweze kunufaika na huduma za Madaktari na Madaktari Bingwa ili kutatua kero za wananchi wanazopata kwa kutafuta huduma ya Madaktari na Madaktari Bingwa kote nchini.

Mbali na hilo, pia inaendelea kushughulikia suala la kuboresha mazingira ya kazi kwa Madaktari na watumishi wa Sekta ya Afya kwa ujumla ikiwa ni pamoja na maslahi yao ili kuwafanya wahamasike kufanya kazi hapa nyumbani badala ya kwenda kufuata maslashi makubwa nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu katika uzinduzi wa huduma za madaktari bingwa mkoani Ruvuma ambako huduma hizo zimewezeshwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

“Changamoto nyingine inayochangia wananchi kutopata huduma za Madaktari Bingwa ni suala la gharama za matibabu na hili litaweza kupatiwa ufumbuzi iwapo mwananchi atakuwa na Bima ya Afya hivyo umefika wakati sasa wananchi wakajiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii(CHF),” alisema Waziri Mwalimu.

Kutokana na hali hiyo, aliuagiza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kuongeza kasi ya kusajili wanachama wapya ili kuwapunguzia wananchi adha ya gharama za matibabu.

Alisema wanachama wa Mfuko huu wanayo fursa ya kupata matibabu mahali popote Tanzania kwa kutumia kadi zao hivyo kila Mtanzania akifanikiwa kuwa na kadi itarahisisha katika upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wote.

“Natoa rai kwa wananchi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, hii itasaidia sana kuboresha huduma na kutatua changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya afya wakati Serikali tukifanya mambo mengine kama ya kuangalia mgawanyo wa madaktari,” alisema.

Katika hatua zingine Waziri alitumia mwanya huo kuhimiza Mamlaka za Halmashauri zote nchini, zihakikishe zinatumia vyanzo mbalimbali vya mapato vinavyotokana na uchangiaji wa huduma za matibabu kutumia fedha hizo kuboresha huduma ikiwemo dawa, vitendanishi na vifaa tiba.