MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umefanya zoezi la uhamasishaji wa huduma yake mpya ya Toto Afya Kadi kwa kutoa elimu ya namna ya kujiunga na kunufaika na huduma hiyo pamoja na kugawa vipeperushi vinavyoelezea huduma zinazotolewa na Mfuko.

Zoezi hilo limeongozwa na Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti Athumani Rehani ambapo maofisa wa Mfuko walihudumia wananchi mbalimbali katika barabara ya Kilwa.

Huduma ya Toto Afya Kadi inalenga kuhudumia watoto ambao ni chini ya umri wa miaka 18 ambao watajiunga na Mfuko kwa gharama ya shilingi 50,400 kwa mwaka ambapo watapata huduma za matibabu kutoka kwenye kitita cha Mfuko.

Akizungumza na wananchi mbalimbali, Bw. Rehani aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo kwa lengo la kuondoa tatizo la kukosa matibabu kwa watoto ambao wengi wameonekana kukosa matibabu wakati wanapougua.

“Hii fursa ni kwa ajili ya watoto kundi ambalo ni kubwa na ni la muhimu kuhakikisha linakuwa kwenye mazingira mazuri ya uhakika wa matibabu hivyo wananchi ni wakati umefika wa kuwaweka watoto katika mazingira mazuri ili waweze kutimiza ndoto zao,” alisema Bw. Rehani.

Kwa upande wa wananchi walipongeza kitendo cha NHIF cha kuingia mtaani kuwafuata wananchi na kuwapatia elimu ya huduma wanazotoa kwa kuwa hatua hii itasaidia watu wengi kuanza kutumia fursa zilizopo.