MWAKA MMOJA WA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

NHIF YAPIGA HATUA KUBWA, YAWAFIKIA WANANCHI

Tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani mwaka 2015 chini ya uongozi wa Rais Dk. John Pombe Magufuli, suala la Afya limekuwa ni moja ya vipaumbele vya Serikali kwa lengo la kuhakikisha uhakika wa matibabu unakuwepo wakati wote kwa wananchi wake.

Rais wetu pia amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi wote kujiunga na Mifuko ya Bima ya Afya ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kufikia lengo la Afya Bora kwa wote.

Mheshimiwa Rais amekuwa akilihimiza hili kwa viongozi na wananchi kama alivyolisisitiza katika siku ya maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi iliyofanyika Mkoani Dodoma.

Katika hotuba yake alisema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha inaweka mazingira yanayowezesha wananchi wengi zaidi wanajiunga kwenye mfumo wa bima za afya. Aliendelea kwa kusema “tunaendelea na juhudi za kupanua wigo wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na pia kuwezesha watumishi wengi wa sekta rasmi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)”.

Tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani imekua na mkakati wa kuboresha huduma za CHF ambapo huduma hizo zitapatikana mpaka ngazi ya mkoa husika lakini pia kutita cha mafao kinaboreshwa ili kukidhi mahitaji halisia na michango inaangaliwa upya. Maandalizi ya kuanza mpango huo yamekamilika na unategemewa kuanza hivi karibuni ambapo hili linakusudiwa kuongeza ufanisi na ubora wa huduma kwani mwanachama atachagua eneo la kujipatia huduma ndani ya mkoa kwa utaratibu wa rufaa.

Jitihada za Mheshimiwa Rais zimeongeza msukumo mkubwa ndani ya NHIF wa kuhakikisha inakuwa na mikakati mbalimbali itakayowezesha Watanzania wengi wanaoendelea kujiunga na Mfuko huu kupata huduma bora zinazokusudiwa.

Kwa usimamizi na ushirikiano mkubwa ambao NHIF inapata kutoka kwa Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu, NHIF imeendelea kupanua wigo wa kusajili wanachama wake lakini pia kuboresha upatikanaji wa huduma kwa waufaika.

Kupanua wigo wa wanufaika wa huduma za NHIF

Tangu kuanza kwa Serikali ya awamu ya tano NHIF imekuwa na ongezeko la wanufaika kwa asilimia 8 ambayo imepelekea kuwa na jumla ya wanufaika 3,528,449 huku CHF ikiwa na ongezeko la asilimia 34 ambayo imepelekea kuwa na wanufaika 9,333,978. Jumla ya wanufaika wa mifuko hii ni 12,862,427 hadi kufikia Septemba 2016.

Ili kuhakikisha urahisi wa upatikanaji wa huduma za matibabu, NHIF imeendelea kusajili vituo vya matibabu ambapo katika kipindi cha Serikali ya awamu ya tano kumekuwa na ongezeko la usajili wa vituo vya matibabu 92 ambavyo vinapelekea kuwa na jumla ya vituo 6,439 vilivyosajiliwa na NHIF hadi kufikia Septemba 2016. Vituo hivi ni vya Serikali, Binafsi na Mashirika ya dini ambavyo viko mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na ni vya ngazi zote kuanzia zahanati hadi ngazi ya taifa pamoja na maduka ya dawa. Hii ni ili kuwawezesha wanufaika wote hata walio vijijini kupata huduma zinazohitajika.

Akizungumzia mafanikio haya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga amesema kuwa lengo la Mfuko huu ni kuendelea kushirikiana na Serikali katika mambo mbalimbali yakiwemo ya uwekezaji katika sekta ya afya ili kuhakikisha suala la matibabu linakuwa na uhakika zaidi na kuondokana na gharama za kupeleka Watanzania nje ya nchi kwa ajili ya huduma ambazo wangeweza kuzipata hapa nchini.

Bw. Konga anasema kwa kuwa Serikali hii ya awamu ya tano ina matazamio makubwa juu ya suala la afya nchini, lazima kuwe na mapinduzi makubwa ndani ya sekta ya afya kupitia mifuko yake katika kipindi cha miaka mitano, hatua itakayoleta kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao. Aliongeza kusema kuwa ni mpango wa Serikali kwamba ifikapo mwaka 2020, asilimia 85 ya Watanzania wanakusudiwa kuwa na bima ya afya.

Makundi Mapya Yanayonufaika na NHIF

NHIF imeendelea kupanua wigo wake kwa kuongaza makundi mbalimbali ya wanufaika na ni katika kipindi cha Serikali ya awamu hii ya tano ambao mfuko umeanza kusimamia upatikanaji wa huduma za matibabu kwa Waheshimiwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Hatua hii ni chachu kubwa katika maendeleo ya Mfuko na sekta ya afya hasa katika uboreshaji wa huduma lakini pia kuwafikia kwa urahisi wananchi wengine ambao viongozi hawa wana hamasa kubwa kwao.

Makundi mengine yaliyofikiwa katika awamu hii ni watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ambao wanaingizwa kwa utaratibu maalum unajulikana kama Toto Afya Kadi. Utaratibu huu umewezesha kila mtoto ambaye hakuweza kusajiliwa kwa taratibu zilizokuwepo awali kujiunga na kunufaika na NHIF.

Mwitikio wananchi katika kujiunga na NHIF na CHF umekuwa ukiongezeka. Pichani watu wakujisajili na CHF Lindi vijijini katika programu za NHIF.

Huduma ya NHIF kwa wamama wajawazito na watoto wachanga.

Changamoto mojawapo katika suala la afya ni Vifo vya wamama wajawazito na watoto hasa katika kipindi cha kujifungua. Serikali kupitia Wizara ya Afya, Mendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na changamoto hii. Kwa kushirikiana na wadau wa afya ambo ni Benki ya Maendeleo ya Ujerumani, NHIF imepanua wigo wa mradi ya mama wajawazito na watoto kwa kuzindua mradi huu katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Upatikanaji wa huduma bora kwa kundi hili kunasaidia kwa kiwango kikubwa kukabiliana na tatizo la vifo vya akina mama wakati wa kujifungua na mpaka sasa Wamama wajawazito takriban 500,000 wamenufaika na mradi huu katika mikoa ya Tanga, Mbeya na mikoa hii mipya ya Lindi na Mtwara tangu mradi huu ulipoanza mwaka 2012.

Akielezea umuhimu wa suala la kupunguza vifo vya akina mama wakati wa kujifungua na watoto chini ya umri wa miaka mitano katika tukio la uzinduzi wa mradi huo mkoani Mtwara hivi karibuni Waziri Mwalimu anasema, lengo namba nne la milenia lilitamka wazi kuwa lazima kila serikali iweke mkakati wa wazi wa kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano. Katika lengo hilo, Tanzania ilifanikiwa kufikia lengo kwa kupunguza kiwango cha vifo vya watoto hadi kufikia vifo 54 kati ya vizazi hai 100,000 (mwaka 2013), kutoka vifo 133 kati ya kila vizazi hai 100,000 (mwaka 2005).

“Kwa sasa tunaweza kujisifu kuwa tumefanikiwa tukilinganisha na idadi ya mwaka 2005 ambapo tulikuwa tunapoteza zaidi ya watoto 133 kati ya kila vizazi hai 100,000. Lakini katika suala la kifo, hata kifo cha mtoto mmoja kinaleta uchungu ule ule ndani ya familia. Hivyo tunatakiwa kuongeza juhudi zaidi ili kuhakikisha kuwa kila mtoto anayezaliwa anaendelea kuishi na kufikia utu uzima kwa kuhakikisha kuwa tunapunguza vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano na watoto wenye chini ya umri wa mwaka mmoja” anasema.

Huduma za madaktari Bingwa maeneo ya pembezoni.

Katika kushiriki jitihada za Serikali ya awamu ya tano, NHIF imefanikiwa kupeleka huduma za Madaktari Bingwa wa magonjwa ya wakinamama, watoto na madaktari wa upasuaji katika mikoa ya pembezoni ambayo wananchi kuanzia ngazi ya kijiji wamenufaika na huduma hizi.

Mfuko umefanikiwa kupeleka huduma hizi katika mikoa ya Kagera, Singida, Ruvuma, Iringa na Njombe ambapo jumla ya wanachama wa Mfuko 1,454 na wananchi wasiokuwa wanachama 2,547 walipata huduma za madaktari Bingwa ambazo kwa hali ya kawaida zingewahitaji gharama kubwa kuzipata mbali na maeneo wanayoishi. Jumla ya wananchi 139 katika mikoa hiyo walipata huduma za upasuaji wa magonjwa mbalimbali hatua ambayo ilileta faraja kubwa katika maeneo hayo.

Kampeni za afya na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.

Ongezeko la wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza imekuwa ni changamoto ambayo Serikali ya awamu ya tano imeivalia njuga kupambana nayo. NHIF pia imekuwa ikishiriki jitihada hizo kwa kuendelea kutoa elimu juu ya magonjwa yasiyoambukiza na kutoa huduma ya upimaji wa magonjwa ya Sukari, Shinikizo la damu, Saratani na suala la Uzito uliokidhiri katika mikutano inayofanya na wadau wake mbalimbali.

Katika utaratibu wake wa elimu Kata kwa Kata, NHIF hufikia kata 560 kwa elimu na upimaji wa magonjwa hayo kwa mwaka kwani kila ofisi ya mkoa ina utaratibu wa kufanya mikutano hii angalao kata tano kila robo mwaka. Lengo kubwa ni utoaji wa elimu ya bima ya afya pamoja na upimaji wa magonjwa yasiyoambukizwa ili kuwaelimisha wananchi wote namna ya kuepukana na magonjwa haya ili wawe na afya njema na hatimaye washiriki kazi za maendeleo ya nchi.

Kituo cha Kisasa cha huduma katika Hospitali ya Rufaa Dodoma kilichozinduliwa hivi karibuni  ya elimu na upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza Mkoani Simiyu hivi karibuni

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu alisema katika uzinduzi wa Kampeni ya Afya yako Mtaji wako iliyoandaliwa na Wizara ya Afya hivi karibuni kuwa suala la kufanya mazoezi na kupima afya ili kujua hali yako ni la msingi na linapaswa kuheshimiwa na kila mtu. Alltaka Wizara kuendeleza kampeni hiyo ili kubadilisha mtazamo wa watu wengi juu ya afya zao.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF akilizungumzia hili katika uzinduzi huo alisema Mfuko unatambua kuwa kampeni hizi zinasaidia watu kutambua afya zao na kuepukana na mtindo wa maisha ambao utapelekea kuwa na magonjwa haya. Aliongeza kwa kusema kuwa elimu hii pia inasaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wanufaika wake kutokana na kupungua kwa wanaothirika.

Uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya afya na vifaa tiba

NHIF imeendlea kuchangia uboreshaji wa huduma za matibabu katika vituo vya kutoleo huduma vilivyosajiliwa na NHIF nchini kwa kutoa mikipo nafuu ya vifaa tiba na ukarabati wa minundombinu ya huduma. Hadi kufikia Septemba 2016, vituo 345 vimenufaika na mikopo hii ambayo huilipa kwa kipindi maalum kupitia madai ya huduma wanazotoa kwa wanachama wa NHIF.

Mbali na mikopo hii, wananchi wanaendelea kunufaika na vituo vya huduma vilivyojengwa kwa uwekezaji wa NHIF kama Hospitali ya Benjamin Mkapa- Dodoma, MOI na kituo cha kisasa katika Hospitali ya Rufaa Dodoma. Katika awamu hii ya tano, ukamilishaji na uzinduzi rasmi wa kituo cha huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma ulifanyika ambapo kituo hicho kimekuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa Dodoma na kutoka nje ya Dodoma. Uwekezaji huu umeleta mabadiliko makubwa ndani ya sekta ya afya hatua itakayosaidia kuondoa gharama kwa Serikali kusafirisha wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Majengo mapya ya MOI yamesadia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Muhimbili kwani yameweza kuongeza nafasi ya kulazwa kwa wagonjwa wa mifupa ambao awali kulikuwa na ufinyu mkubwa wa nafasi za kulaza.

 

Mojawapo ya mikutano ya kampeni ya elimu na upimaji wa magonjwa yasiyoambukizwa mkoani Simiyu.