TUTASHIRIKIANA NA WADAU WETU KULETA MAPINDUZI YA HUDUMA ZA NHIF KWA MWAKA 2017 - KAIMU MKURUGENZI MKUU

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bw. Bernard Konga amewahakikishia wanachama, wadau na Watanzania kwa ujumla kuwa NHIF itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha mwaka 2017 unakuwa ni mwaka wa mafanikio makubwa kihuduma.

Amesema kuwa NHIF ina dhamana kubwa ya kutoa huduma bora kwa wanachama wake lakini pia kuhakikisha inashiriki kikamilifu katika uboreshaji wa huduma za afya nchini kwa kushirikiana na Serikali.

“Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wadau wetu kwa ushirikiano ambao mmekuwa nao katika huduma zetu, nyie mmekuwa ni chachu kubwa ya kuleta mabadiliko na maboresho mengi hivyo niahidi tu kwamba mwaka 2017 ni mwaka ambao Mfuko umejipanga vyema kutoa huduma bora zaidi".

Katika mwaka 2016 Mfuko umeweza kupanua wigo wa wanufaika, kuboresha kitita cha mafao lakini pia kuimarisha mifumo ya utendaji kutumia TEHAMA ili kuleta ufanisi kwenye usajili, utoaji vitambulisho na ulipaji madai.

Bw. Konga ametumia fursa hii kuwatakia kila la heri wadau wake na Watanzania kwa ujumla katika kumaliza mwaka 2016 na kuingia mwaka 2017 wakiwa na afya njema, amani na utulivu.

Amesema kuwa kutokana na dhamana kubwa ambayo NHIF inayo katika suala la upatikanaji wa huduma za matibabu, itaendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa bima ya afya kwa Watanzania, ili hatimaye kila mtu aweze kunufaika. NHIF itaendelea kuwahimiza Watanzania juu ya umuhimu wa kuishi mtindo bora wa maisha ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na saratani.

Alimaliza salamu zake kwa kuwataka wanachama na wadau wote kwa ujumla kuendelea kutoa mrejesho wa huduma kupitia kituo cha huduma kwa wateja kwa namba 0800 110063 lakini pia mikutano ya mara kwa mara ambayo NHIF inafanya na wadau wake. Alisema mrejesho huo ni wa maana sana katika kupelekea maboresho na huduma bora zaidi.