• Yadhamiria kuimarisha ubora wa huduma zake

  • “Ubora wa huduma za NHIF unategemea uwajibikaji wa kila mdau”

“Tutafanya kazi na watoa huduma walio tayari kutoa huduma bora kwa wanachama wetu”. Maneno haya aliyasema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bi. Anne Makinda wakati wa mikutano ya wadau wa NHIF iliyofanyika katika mikoa ya Kanda ya ziwa.

Akizungumza na wadau hao kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu, Kagera, Geita na Kigoma Bi. Makinda alisema bodi yake imeamua kupita kila mkoa kukaa na wadau ili kupata mrejesho wa huduma za Mfuko huo, kuzijadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo kwa pamoja. Wadau hao wa Mfuko walioshiriki mikutano hiyo ni pamoja na Viongozi wa Serikali za mikoa hiyo, watoa huduma za afya waliosajiliwa na Mfuko huo, waajiri, wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi na wanachama.

Mfuko wa Taifa wa bima ya afya unatoa huduma kwa wanachama wake ambao huchangia kabla ya kuugua na kisha kupata huduma za matibabu kutoka vituo vya matibabu 6,998 nchi nzima ambavyo vimesajiliwa na NHIF kwa sasa. Ufanisi wa Mfuko huu unategemea kwa kiasi kikubwa uwajibikaji wa kila mdau. NHIF hukusanya michango na kulipia huduma za matibabu kwa watoa huduma ambao wamewahudumia wanachama wa NHIF kila mwezi. Kutokana na mfumo huo, kutokuwajibika kwa baadhi ya wadau husababisha changamoto za ubora wa huduma kwa wanachama wa NHIF. Changamoto kubwa inayojitokeza na kujadiliwa ni huduma zisizoridhisha zinazotolewa na baadhi ya watoa huduma ambao wameingia mkataba na NHIF kuwahudumia wanachama wake.

Akiongelea suala hili katika mikutano hiyo, Bi Makinda alihoji “…..kuna gharama kiasi gani kwa wewe mtoa huduma kuwa na kauli nzuri kwa mgonjwa, au unapata faida kiasi gani kwa kutoa kauli chafu kwa mgonjwa aliyekuja kituoni kwako kupata huduma?”

Bodi ya NHIF ilionesha kukerwa sana na watoa huduma ambao wameingia mikataba na NHIF kuwahudumia wanachama wake kulingana na vigezo vilivyowekwa lakini wanakuwa na huduma mbaya na kutoa huduma kinyume cha makubaliano yaliyopo baina yao. Wakiongea kwa nyakati tofauti, Wajumbe wa Bodi ya NHIF ambao walishiriki mikutano hiyo Bw. Tryphon Rutazamba, Dk. Baghayo Saqware na Bi. Lydia Choma wakiongozwa na Mwenyekiti wao walisema Mfuko utafanya kazi na watoa huduma ambao wako tayari kuwajibika na kutoa huduma bora kwa wanachama wa Mfuko kulingana na makubaliano yaliyopo. “ Hatutasita kusitisha mkataba na watoa huduma wanaonyanyasa wanachama wa NHIF kwa sababu ambazo ziko nje ya makubaliano yetu, sisi tutakuwa tayari kukaa pamoja nanyi na endapo kuna changamoto tuzijadili na kurekebisha kwa pamoja lakini sio kunyanyasa wanachama wa Mfuko huo” alisema Bi. Makinda.

Akiongea katika Mkutano wa wadau mkoani Geita, Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga alisema kuna haja ya kujipanga upya kuhakikisha huduma bora zinapatikana katika vituo vyetu vya huduma hasa kwenye suala la ufuatiliaji wa huduma zinazotolewa na wahudumu katika vituo vya afya. “Nitafuatilia kuhakikisha wahudumu katika vituo vyetu vya huduma wanatoa huduma zinazofaa kulingana ni miongozo waliyonayo, sitawavumilia watoa huduma ambao wamekuwa wakitoa lugha zisizofaa na kinyanyasa wagonjwa katika vituo vyetu kinyume na miongozo ya taaluma zao, tutawashughulikia”

Wakati akitoa mada ya taarifa utekelezaji na maboresho ya shughuli za Mfuko, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga alisema NHIF imefanya maboresho mengi katika huduma zake kwa kushirikiana na wadua. “Hivi karibuni tumepitia upya na kuboresha kitita cha mafao na bei ya huduma za NHIF kwa kushirikiana na wadau hasa watoa huduma ili kuhakikisha mtoa huduma anapata haki yake na mwanachama anapata huduma bora” Aliongeza kusema kuwa Mfuko umeendelea kutoa mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa miundombuni kwa vituo vya huduma ili kuhakikisha huduma zinaboreshwa. Aliutaka ungozi wa Serikali za Mikoa kuhimiza vituo vyao kuchangamkia fursa hii ili kuboresha huduma.

Akiliongelea hili, Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk. Charles Mlingwa alimuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa kufuatilia mahitaji ya vifaa tiba yaliyopo katika vituo vyake na kuhakikisha fursa hii inatumika mara moja. “….unajua mwanachama wa NHIF anachagua kituo cha kumhudumia kwa sababu kadi yake haina pingamizi antumia mkoa wowote na kituo chochote kilichosajiliwa. Kama kituo chako kina huduma mbaya, hakina vifaa tiba, basi hutawapata hawa na matokeo yake utakosa mapato ya kutosha. Naomba RMO unipatie ripoti ya mahitaji ya vifaa katika vitoa vyetu na uwezo wao wa kukopa ili tuweze kuitumia fursa hii vema zaidi na kuboresha huduma”

Akihitimisha mkutano wa wadau Mkoani Geita, Bi. Makinda allisema, Bodi yake imedhamiria kufanya maboresho makubwa katika huduma kwa wanachama wake na kwamba imetengeneza vipaumbele kadhaa vya utekelezaji katika kipindi cha uongozi wao mojawapo ikiwa ni kuhakikisha wanashirikiana na wadau husika kuhakikisha huduma kwa wanachama wa NHIF zinaboreshwa kwa kiwango kikubwa. “ Tumeweka vipaumbele vya utekelezaji wetu na tutafanya kazi na ninyi wadau kwa karibu ili kuhakikisha huduma zinaboreshwa. Hatutaishia hapa, tutafika pia na mikoa mingine, kusudi ni kuhakikisha tunasimama na serikali za mikoa na wadau katika mikoa husuka ili kuhakikisha huduma bora zinapatikana” alisema Mwenyekiti hiyo wa Bodi ya NHIF.

 

Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF Mheshimiwa Anne Makinda akiongea na wadau wa NHIF Mkoani Njombe

   Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Benard Konga akiwasilisha mada kwenye mkutano wa wadau mkoani Mara

         Wadau mbalimbali wa NHIF wakifuatilia mada katika mkutano wa wadau mkoani Kigoma

    Mjumbe wa Bodi ya NHIF Dk. Baghayo Saqware akitoa ufafanuzi wa jambo katika mkutano wa wadau wa NHIF mkoani Kigoma.