NHIF Kilimanjaro Kudhibiti Udanganyifu kwa Kuboresha Ushirikiano na RITA

Imewekwa: 16 April, 2026
NHIF Kilimanjaro Kudhibiti Udanganyifu kwa Kuboresha Ushirikiano na RITA

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

Katika kuboresha huduma za usajili wa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Uongozi wa Mfuko umeombwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Mamlaka ya Vizazi na Vifo (RITA) ili kuweka mikakati ya udhibiti wa nyaraka mbalimbali zinazotumika katika uhakiki wakati mwanachama anaposajiliwa na Mfuko.

Rai hiyo imetolewa jana Aprili 14, 2026 na Watumishi wa NHIF Mkoa wa Kilimanjaro mbele ya Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko inayoongozwa na Bw. Eliud Sanga ambayo ilikuwa mkoani hapo wakati wa ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa shughuli za kuwahudumia wanachama kwa ngazi ya Mkoa.

Akiwasilisha ombi hilo Msimamizi wa Ofisi ya NHIF Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Petronida Ndagala, alisema kuwa changamoto kubwa wanayokutana nayo wakati wa kuwasajili wanachama ni nyaraka za kughushi ambazo ni vyeti vya kuzaliwa na vyeti vya ndoa hali inayosababisha usumbufu mkubwa na upotevu wa muda.

“Tunashukuru sana kwa mifumo yetu kusomana na RITA pamoja na NIDA ambayo kwa kiwango fulani inatusaidia kubaini nyaraka mbalimbali wanazokuja nazo wananchi kwa ajili ya usajili, lakini tunaomba kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kudhibiti wimbi kubwa ambalo limejitokeza la kubadilisha majina kwenye vyeti ili yafanane na yaliyoko kwenye NIDA hii inasababisha wengi kujihusisha na vitendo vya kughushi nyaraka,” alisema Bi. Ndagala.

Meneja wa NHIF Mkoa wa Kilimanjaro akipokea maelekezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Bw.Eliud Sanga wakati wa ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro tarehe 14 April,2026

Aliongeza kuwa NHIF kuendelea kushirikiana na taasisi hizo itasaidia kuweka mikakati ya kubaini na kudhibiti mianya ya udanganyifu kupitia nyaraka zinazowasilishwa kwenye Mfuko kutoka kwenye taasisi hizo.

Akijibu hoja mbalimbali Mwenyekiti wa Bodi Bw. Sanga aliwapongeza watumishi kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuahidi kuwa masuala ya kisera yaliyowasilishwa kwao watayafanyia kazi ili kuhakikisha watumishi wanatekeleza majukumu yao bila vikwazo vyovyote.

Aliwataka Watumishi wa Mfuko kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanafikia wananchi wengi zaidi na kutimiza azma ya Serikali ya kila Mtanzania kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha.

Katika ziara hiyo inayohusisha mikoa ya Singida, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga, Mwenyekiti wa Bodi ameongozana na Prof. George Luhago pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka.

Watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wakifuatilia kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wakati wa ziara ya kikazi iliyofanyika mkoani humo

Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge sasa