Mkurugenzi wa Huduma za Uanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt. Alphonce Chandika, amesema mfuko umefurahia fursa ya kukutana na viongozi wa wachimbaji mkoani Geita kwa lengo la kutoa elimu na kushirikiana nao katika kuhamasisha wanachama kusajiliwa kwenye bima ya afya.
Dkt. Chandika alieleza kuwa ni muhimu kuwashirikisha viongozi hao kwanza, ili kupitia wao, ujumbe uweze kuwafikia wachimbaji wengi zaidi. Alibainisha kuwa mfuko una utaratibu wa waajiri kusajili wafanyakazi wao moja kwa moja kupitia ajira, lakini pia kuna vifurushi vya bima ya afya ambavyo mtu binafsi anaweza kuvichagua kulingana na mahitaji yake na kupata huduma za matibabu kupitia NHIF. Aliyasema hayo baada ya kukutana na viongozi wa wa Vyama vya Wachimba Madini Mkoani Geita akiambatana na Meneja wa NHIF wa Mkoa huo Bw. Elius Odhiambo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Mkoa wa Geita, Bw. Titus Kabuo, alisema huduma ya bima ya afya ni muhimu kwa wanachama wao na kuongeza kuwa ili kufanikisha jambo hilo, ni lazima wachimbaji wapate uelewa wa kutosha kuhusu taratibu na namna ya kunufaika na huduma hizo.
Katika kikao hicho, Bw. Kabuo aliiomba NHIF kupanga vikao vya pamoja na chama hicho ili kutoa elimu zaidi kwa wachimbaji. Alifuatana na Bw. Misana Nyabange, Katibu wa chama hicho, pamoja na Bi. Evelyne Nzinza, Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Geita.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa