Timu ya wanawake ya mpira wa pete (netiboli) ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) imefanikiwa kutwaa kombe la mshindi wa kwanza katika mashindano ya OSHA yaliyofanyika mkoani Njombe, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya OSHA. Ushindi huo umeonyesha kiwango cha juu cha ushindani dhidi ya timu zilizoshiriki mashindano hayo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi, Kamishna wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Suzan Mkangwa, alisema kuwa bonanza hilo lina faida kubwa kwa watumishi, ikiwemo kuongeza ufanisi kazini, kuleta wafanyakazi pamoja na kuimarisha mshikamano. Alibainisha kuwa michezo huchochea motisha kazini, huboresha mawasiliano, na kuwajengea watumishi uwezo wa kusikilizana pamoja na kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali kwa ubunifu.

Aidha, aliongeza kuwa taasisi zinazothamini michezo huwa na wafanyakazi wenye ari na morali ya juu ya kazi, hali inayochangia kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila sikuna pia kuendeleza mapambano dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCD’s).
Naye kwa upande wake Nahodha wa timu hiyo, Bi. Jacqueline Sikozi akizungumza kwa niaba ya wachezaji wote wa timu ya netiboli alitoa shukurani kwa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene Isaka kwa kuwezesha ushiriki wa watumishi katika michezo ya Mei Mosi ambayo imekuwa ni sehemu ya kujiimarisha kiafya na kiakili.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa!