Health Insurance for Private Individuals

MWANACHAMA BINAFSI NI NANI?

Mwanachama binafsi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, ni mtu yeyote anayeamua kujiunga na Mfuko huu kwa hiari bila uwepo wa uhusiano baina ya mwajiri na mwajiriwa.

WANUFAIKA WA UTARATIBU HUU

Mwanachama binafsi atapata fursa ya kuwa na wategemezikama ilivyo kwa mwanachama aliyeajiriwa. Wategemezi wanaokubalika ni wale tu wanaotambulika kisheria chini ya utaratibu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Wategemezi hawa ni pamoja na mwenzi wa mchangiaji, (mke au mume), watoto wa kuzaa au kuasili au wazazi wa pande zote mbili.

UTARATIBU WA KUJIUNGA

Masuala yafuatayo ya msingi lazima yazingatiwe kabla ya kuanza kujiandikisha;-

  • 1)Mwombaji atajaza fomu ya maombi ya uanachama binafsi
  • 2)Mwombaji lazima adhaminiwe na mwanachama wa Mfuko huu aliye ajiriwa serikalini;
  • 3)Mwombaji lazima ajaze fomu ya uanachama ikiambatanishwa na picha mbili za pasipoti za rangi za kwake na kila mtegemezi anayetambulika kisheria;
  • 4)Wakati wa kuandikisha wategemezi mwombaji lazima awasilishe nyaraka za kisheria zinazoonesha uhusiano wake na wategemezi aliowaainisha.
  • 5)Vitambulisho vya matibabu vitatolewa kwa kila mtegemezi atakayeainishwa na vitakuwa na ukomo wa mwaka mmoja.
  • 6)Kila mwisho wa muda wa matumizi wa vitambulisho husika, mwanachama atatakiwa kuomba upya uanachama kwa kuchangia kiwango cha mchango kitakachowekwa na Mfuko kwa wakati huo;
  • 7)Mwanachama ataanza kupata huduma baada ya siku 21 za kujiunga.

UTARATIBU WA UCHANGIAJI KWA MWANACHAMA BINAFSI

Mwanachama binafsi atachangia kiwango kilichowekwa na Mfuko kwa mkupuo mmoja kila mwaka kabla ya kuanza kupata huduma.

UKOMO KWA MWANACHAMA BINAFSI

Mwanachama binafsi na wategemezi wake walioandikishwa, uanachama wao utakoma:-

  • I.Endapo mwanachama mchangiaji atafariki, hata hivyo wategemezi wa mwanachama wataendelea kupata huduma kwa kipindi kilichosalia ndani ya mwaka husika;
  • II.Endapo hatachangia upya kwa awamu inayofuata.