Akizungumzia mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema “Mwananchi anapokuwa na kadi ya bima ya afya anapata huduma za matibabu bila malalamiko yoyote kuliko mwananchi anayepata huduma bila kuwa na kadi, hivyo hiki ni kipaumbele changu kwa muda nitakaokuwa ndani ya Wizara hii,” amesema Waziri Ummy.
Ametumia mfano wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo asilimia 80 ya wagonjwa wake ni wanachama wa NHIF ambao wanapata huduma za matibabu bila ya kuwa na malalamiko yoyote.
“Serikali imeshawekeza sana katika sekta ya afya na kilichobaki kwa sasa ni kusimamia upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi na upatikanaji wa bima ya afya ili kurahisisha huduma hizo, tunaamini suala la bima ya afya kwa wote lilipofikia ni pazuri na tutakwenda nalo bungeni mwezi Septemba ili sheria hii ianze kutumika,” alisema Mhe. Ummy.
Kwa upande wa NHIF ambayo kwa sasa inahudumia asilimia nane ya Watanzania wote, inaendelea na mpango wake wa kuwafikia wananchi wengi zaidi ili waweze kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu.
Mkurugenzi Mkuu Bwana Bernard Konga amesema kuwa, NHIF imeweka utaratibu kwa kila kundi na kila mwananchi unaomwezesha kujiunga na kunufaika na Mfuko umefanikiwa kuwa na mtandao mpana wa vituo vya kutolea huduma za matibabu Tanzania Bara na Zanzibar.
Mwisho.