. Yajifunza utoaji bora wa huduma kwa wanachama
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umepongezwa kwa uwekezaji mkubwa ilioufanya kwenye eneo la mifumo ambayo imerahisisha utoaji wa huduma kwa watoa huduma na wanachama wake.
Hayo yalisemwa jana na Prof.Omar Jah Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wa Jamhuri ya Gambia akiwa ameongozana na Katibu Mkuu Wizara ya Jinsia na Maendeleo ya Jamii Bi.Rohiatou Kah.
Ujumbe huo kutoka Gambia wakiwemo Wakuu wa Taasisi, upo nchini kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu na NHIF katika eneo la bima ya afya.
Alisema kuwa mfumo uliopo na unaotumika kwenye mnyororo wa kuwahudumia wadau wa NHIF umezingatia mahitaji ya msingi katika utoaji wa huduma bora na haraka kwa wanachama na wadau wengine.
“Mmefanya mambo makubwa tunaona tumekuja sehemu sahihi, kila eneo la utendaji lina matokeo kwa mwanachama na ndiyo sababu mnaendelea kuwa Mfuko wa mfano katika ukanda huu wa Bara la Afrika hususan kusini mwa Jangwa la Sahara, hongereni Sana na
Sisi tunaenda kuyatekeleza yote na tutaendelea kujifunza kutoka kwenu,” alisema Prof. Omar.
Akizungumza na ugeni huo, Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Bw. Sanga ameelezea mikakati iliyopo na namna Mfuko ulivyojipanga katika kuwafikia wananchi wote. Mikakati iliyopo ni pamoja na kampeni za uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa wananchi, kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo benki, makampuni ya simu, mawakala na wadau wa maendeleo.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka, amewashukuru wageni kwa kuichagua Tanzania ili kujifunza mifumo ya uendeshaji wa bima na ameahidi kuendeleza mashirikiano zaidi kati ya pande zote mbili.
“Tuko kwenye utekelezaji sasa wa bima ya afya kwa wote, naamini yatakuwepo mazuri mengi ya kuja kujifunza kwetu,” alisema Dkt. Irene.
Mbali na hayo, wageni hao wamepata elimu juu ya Sheria iliyoanzisha Mfuko na maboresho yake, makundi yanayonufaika kupitia vifurushi mbalimbali vinavyotolewa na Mfuko, adhma ya serikali kuelekea utekelezaji wa bima ya afya kwa wote na wametembelea baadhi ya Vituo vya kutolea huduma vilivyosajiliwa na Mfuko kwa lengo la kuona namna huduma zinavyotolewa kwa wanachama na uwasilishaji wa madai kwa NHIF.