HALMASHAURI KUU CCM YARIDHIA MAPENDEKEZO YA BIMA YA AFYA KWA WOTE

HALMASHAURI KUU CCM YARIDHIA MAPENDEKEZO YA BIMA YA AFYA KWA WOTE Jun 24, 2022

Halmashauri Kuu ya Taifa CCM (NEC) imeridhia mapendekezo ya Bima ya Afya kwa wote nchini kwa kuwa itasaidia wananchi katika uhakika wa huduma za matibabu.

NEC ambayo iliketi jana mkoani Dodoma na Wajumbe wote kupitisha kwa kishindo mapendekezo hayo kwenye semina iliyoandaliwa na Wizara ya Afya iliyolenga kuimarisha mfumo wa bima ya afya nchini.

Akizungumzia kuridhiwa kwa mapendekezo hayo, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hatua hiyo inapelekea Wizara kwenda kutunga sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.

Aliongeza kuwa kiasi kitakacholipwa na mwananchi kwa mwaka kitamsaidia kupata huduma za matibabu kama ilivyo kwa mtumishi wa Serikali, kuanzia ngazi ya Zahanati, Kituo cha Afya, hospitali za Wilaya, Rufaa za Mkoa, Kanda na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

"Hii itasaidia kwa Watanzania wote kupata huduma bora za Afya bila kikwazo cha fedha pia Serikali itahakikisha Dawa zinapatikana kwa wakati na zinazokidhi mahitaji ya wagonjwa". Amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy amesema kuwa na bima ya afya kwa wote ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, Ibara ya 83(e) kwa kuimarisha mfumo wa bima ya afya nchini ikiwemo mifuko ya bima za afya (NHIF na CHF) ili kufikia lengo la Serikali la kuwa na bima ya afya kwa wananchi wote.

Akiwasilisha mada ya Mapendekezo ya kuimarisha Mfumo wa Bima ya Afya nchini kwa wajumbe wa NEC, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bw. Bernard Konga alisema kuwa sheria hiyo itasaidia kuwepo kwa utaratibu unaomwezesha mwananchi kupata huduma popote nchini tofauti na ilivyo sasa kwa baadhi ya bima ya Afya.

"Hii itasaidia sana kwa mwananchi kupata huduma katika vituo vyote vya Serikali na binafsi na mahali popote, hivyo sheria hii inakwenda kuondoa malalamiko mengi ya wananchi" alisema Bw. Konga.

Faida nyingine aliitaja kuwa ni kuwapa wananchi wote kitita cha mafao kitakachowiana, hatua inayokwenda kuleta usawa na kuondoa matabaka.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Mhe. Christina Mndeme akifungua kikao hicho aliishukuru Serikali kwa kuwashirikisha Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kutoa maoni katika mapendekezo ya kuimarisha mfumo wa bima ya afya nchini.

Akihitimisha mkutano huo, Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda aliipongeza Serikali kwa hatua hiyo na kuhimiza suala hilo liweze kugusa maisha ya wananchi wa kipato cha chini.

Mwisho.