Hatutaruhusu kupata huduma bila ya kuwa na kadi - Konga

Hatutaruhusu kupata huduma bila ya kuwa na kadi - Konga Sep 16, 2021

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bw. Bernard Konga ameweka wazi kuwa Mfuko hautaruhusu matumizi ya huduma za matibabu kwa mwanachama atakayefika kituoni bila ya kuwa na kitambulisho cha matibabu.

Amesema kuwa, Mfuko unamtambua mwanachama wake kupitia kitambulisho chake ambacho anakitumia kwenda kwenye vituo mbalimbali vilivyosajiliwa kwa lengo la kupata huduma.
“Kadi ya NHIF ni muhimu kama zilivyo kadi za huduma zingine kama benki na pale inapopotea mwanachama husika anatakiwa kuzingatia taratibu zilizopo ikiwemo ya kuwa na taarifa ya kupotea kutoka Polisi ili apatiwe kitambulisho kingine,” alisema Bw. Konga.

Hayo ameyasema leo katika Mkutano wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (COTWU(T) wakati akiwasilisha mada iliyohusu utekelezaji wa Mfuko katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.

Amesema kuwa kwa sasa Mfuko umejiimarisha zaidi katika udhibiti wa vitendo vya udanganyifu katika huduma zake hivyo kila mwanachama anatakiwa kufika katika kituo cha kutolea matibabu akiwa na kadi yake na atatambuliwa na Mfumo endapo ana uhalali wa kupata huduma au la.
“Niwaombe sana ili Mfuko wetu uendelee kuwa na nguvu na kutoa huduma nyingi na bora tunazozihitaji ni lazima tushirikiane kwa pamoja katika kuulinda Mfuko wetu, tunakubali kuwa zipo dharula zinazowapata wanachama wetu na tumeweka utaratibu mzuri kabisa wa kuwawezesha kupata huduma mara tu wanapowasiliana nasi" alisema.

Akizungumzia kanuni za utoaji wa huduma za NHIF, alisema wanachama wanajiunga kwa mujibu wa Sheria ambapo michango yao huwekwa kwenye kapu moja ambalo linawezesha kila mwanachama kupata huduma sawa bila kuangalia utofauti wa michango yao.
“Kanuni nyingine ni kutoa huduma kwa wananchi na si kupata faida kama zilivyo bima za afya binafsi hivyo uendelevu na uimara unategemea uchangiaji kutoka kwa kundi kubwa la wananchi lakini pia matumizi sahihi ya huduma ambayo yanauwezesha Mfuko kulipa fedha halali,” alisema.

Akizungumzia suala la wategemezi, alisema kuwa kwa sasa Mfuko unawatambua wategemezi wa mwanachama kuwa ni watoto wake, wazazi wake ama wakwe zake katika nafasi alizopewa hivyo akawaomba kuendelea na utaratibu huo na endapo kutakuwa na mabadiliko wanachama watajulishwa.
Alitumia fursa hiyo pia kueleza kuwa Mfuko unatarajia kuzindua Mfumo ‘APP’ itakayomwezesha mwanachama kupata taarifa mbalimbali zikiwemo za vituo na ngazi ya huduma anayotaka kupata lakini pia taarifa za kadi yake na ukomo wa matumizi ya kadi hiyo.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa COTWU (T), Bi. Juliana Mpanduji aliupongeza Mfuko kwa huduma inazozitoa kwa wanachama wake lakini pia kushirikisha wadau katika kutoa maoni ya namna ya uboreshaji wa huduma zake.
Mfuko kwa sasa uko katika maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake ambapo unakutana na wadau wake wakiwemo wanachama, vyama vya wafanyakazi, watoa huduma za matibabu, wanahabari na makundi mengine kwa lengo la kupokea mrejesho wa huduma na kuwapa taarifa za utendaji wake katika miaka 20.

Mwisho.