Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF leo umezindua kampeni ya kuhamaisha wananchi kujiunga na mpango wa vifurushi katika Mkoa wa Kilimajaro.
Katika uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mama Anna Mghwira ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwataka watanzania kujiunga na NHIF ili kuwa na uhakika wa matibabu badala ya kusubiri kuumwa ndipo waanze kutafuta kadi ya bima ya afya.
“Wakati wa amani ambao ni wakati upo mzima unatakiwa uwekeze na NHIF kwa kukata kadi ya Bima ya Afya na wakati wa vita ambao ni wa maradhi NHIF ni wa uokoaji kwa kujitibia, jiungeni na NHIF ili tuwe na uhakika wa matibabu”-Amesema RC Mghwira
Aidha, RC Mghwira ameupongeza Uongozi wa NHIF pamoja ma Bodi ya Mfuko huo kwa kuja na mpango huu wa vifurushi vya Bima ya Afya ambao una lengo la kuwajumuisha watanzania wengi zaidi.
Akiongea katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF Mama Anne Makinda amesema kuwa Mpango wa vifurushi vya Bima ya Afya hauzuii taratibu nyingine za Serikali ikiwemo Sera ya Afya inayotambua afya bure kwa watu wasio na uwezo ikiwemo Wazee.