Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Stephen Kagaigai ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kazi kubwa inayofanya na kwa ushirikiano inayotoa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Bunge.
Amesema NHIF ni taasisi ambayo imekuwa tegemeo kwa afya za Watanzania hivyo akatoa rai kwa wanachama wote na watumishi kuhakikisha wanaulinda Mfuko huo ili uweze kuimarika na kutoa huduma zaidi kwa vizazi na vizazi.
Hayo aliyasema Dar es Salaam jana wakati akizungumza na Mkurugenzi Mkuu na baadhi ya Maofisa wa Mfuko waliohudhuria uzinduzi wa Michezo ya wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Huu Mfuko kwa kweli umekuwa ni msaada sana kwetu, nawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayoifanya na kipekee nitoe pongezi zangu kwa namna mnavyoshirikiana na Bunge letu katika kuhakikisha huduma tunapata kama inavyotakiwa,” alisema Bw. Kagaigai.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Konga alisema kuwa Mfuko utaendelea kuboresha na kuimarisha huduma zake ili kila Mwananchi ajivunie uwepo wa Mfuko huu kwa kuwa ni njia bora ya kupunguza gharama za matibabu.
Alisema kuwa Mfuko umeshiriki kikamilifu katika mashindano hayo ya michezo kwa kuhakikisha huduma za awali za matibabu pamoja na vipimo kwa wabunge vinapatikana wakati wote wa michezo.
“Tumeshirikiana na Ofisi ya Bunge kuhakikisha afya za waheshimiwa wabunge zinakuwa imara wakati wote wa michezo na huduma zitatolewa kwa wabunge wote bila kujali nchi aliyotoka kwa kuwa sote tunaunganishwa na Jumuiya hii ya Afrika Mashariki,” alisema Bw. Konga
Alitumia fursa hiyo pia kuwaomba wananchi watakaofika katika Uwanja wa Taifa kutembelea banda la Mfuko ambalo watapata elimu mbalimbali juu ya huduma zinazotolewa na Mfuko.
Mwisho.