Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa ameipongeza NHIF kwa uboreshaji wa huduma za usajili wa wananchi kidigitali alipotembelea banda lao wakati Ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha leo jijini Arusha.
Ameyasema hayo alipokua akipata maelezo ya namna NHIF ilivyojipanga kuwafiki wananchi wengi zaidi kwa kutumia njia za kidigitali ambapo mpaka sasa mwanachama anaweza kuhuisha uanachama wake kwa simu yake bila kulazimika kufika ofisi za NHIF.
"Niwapongeze kwa jitihada mnazofanya kuwafikia wananchi mpaka vijijini hasa kipindi hiki tunapohitaji kila mtanzania aweze kuwa na bima ya afya" alisema Mhe Majaliwa
Awali akitoa maelezo kuhusu ya ushiriki wa NHIF kwenye maadhimisho hayo, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Meneja Uhusiano wa NHIF Bi. Anjela Mziray alisema Mfuko unatoa elimu kwa wananchi ili wawekeze kwenye afya zao kwa kuchangia kwenye bima ya afya kabla ya kuugua ili wawe na uhakika wa matibabu bila kikwazo watakapougua.
Aidha, Bi Anjela alielezea namna Mfuko ulivyojipanga kurahisisha huduma zake kidigitali kwenye usajili wa wanachama, watoa huduma na waajiri na kufanya malipo bila ulazima wa kufika kwenye ofisi za Mfuko.
"Serikali imeshawekeza sana kwenye miundombinu na upatikanaji wa huduma za afya mpaka vijijini na tuko hapa kuwaelimisha wananchi wajiunge na bima ya afya ili waweze kuzipata huduma hizo" amesema Bi. Anjela
Awali alipotembelea banda la NHIF Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Pro. Joyce Ndalichako alipongeza huduma za elimu na usajili wa wanachama zinazofanywa kwenye banda hilo