Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umeanza kutumia Mifumo ya TEHAMA katika katika kusajili, kutambua wanachama na malipo ya michango ambapo wanachama hawalazimiki kufika ofisini za Mfuko.
Matumizi hayo ya mifumo yatamuwezesha mwanachama kutumia namba yake ya NIDA au kitambulisho cha kielektroniki (eCard) kupata huduma za matibabu katika vituo vilivyosajiliwa na Mfuko nchi nzima.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka wakati wa halfa ya uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa soko la Bima la Mwaka 2023 ulioshirikisha wadau mbalimbali wa bima nchini.
Alisema kuwa katika kuongeza wigo wa wanachama hususan wakati huu wa utekelezaji wa sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Mfuko utashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo mabenki na kampuni za simu kuwafikia wananchi kwa wingi na kwa njia rahisi pamoja na kufanya uhamasishaji kupitia njia mbalimbali ikiwemo maonesho ya kitaifa na kimataifa, masoko, nyumba za ibaada, vyombo vya habari na matangazo.
“Mfuko umeandaa vifurushi vya bima ya afya kwa kuzingatia ukubwa wa familia, aina ya huduma, umri na uwezo wananchi kuchangia ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kujiunga kuanzia mtu mmoja hadi familia lakini pia tumeandaa kifurushi cha bima ya afya cha huduma za ziada (supplementary package) kwa kuzingatia mahitaji ya mwajiri na uwezo wa kugharimia nah ii inamsadia mwananchi kuchagua,” alisema Dkt. Isaka.
Akizungumzia huduma bora kwa wanachama, alisema Mfuko unahakikisha huduma anazopewa mwanachama zimefuata miongozi ya tiba nchini (Standard Treatment Guidelines) na kuendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu ya ukarabati wa vituo, vifaa tiba, dawa na TEHAMA kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma bora katika vituo vilivyosajiliwa na Mfuko.
Kutokana na hayo, amewaomba wananchi kujiunga na huduma za Bima ya Afya ili kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote bila kikwazo cha fedha.
*Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa*