NHIF YAPONGEZWA NA WATOA HUDUMA ZANZIBAR

Imewekwa: 30 January, 2025
NHIF YAPONGEZWA NA WATOA HUDUMA ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) leo Januari 30, 2025 umefanya mkutano na watoa huduma za afya wenye vituo binafsi na za Serikali, waliopo Zanzibar, kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utoaji wa huduma kwa wanachama wa mfuko huo.

Akifungua mkutano huo, Meneja wa NHIF Mkoa wa Temeke Bw. Cannon Luvinga, aliwasilisha salamu za Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka, ambapo alieleza kuwa Mkurugenzi Mkuu anathamini na kupongeza juhudi za vituo vya afya vya serikali na binafsi vinavyohudumia wanachama wa NHIF Zanzibar.

“Mkurugenzi Mkuu anawapongeza kwa kazi nzuri inayofanywa na vituo vyenu katika kuokoa maisha ya Watanzania, hasa wanapohitaji matibabu. NHIF pia imefanya maboresho makubwa kwenye mifumo ya malipo, ambayo inarahisisha uchakataji wa madai na kuhakikisha malipo yanafanyika kwa wakati,” alisema Bw. Luvinga.

Katika mkutano huo, watoa huduma zaidi ya 45 walipata fursa ya kujifunza miongozo ya matibabu, pamoja na maboresho yaliyofanywa na NHIF kwenye mifumo ya usajili na uchakataji wa madai. Lengo lilikuwa kuwakumbusha watoa huduma kuhusu umuhimu wa kufuata miongozo hiyo ili kuepuka makato yanayosababishwa na kutofuata taratibu sahihi.

Watoa huduma walieleza kuridhika kwao na NHIF kwa kuandaa kikao hicho, na walikiri kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa zaidi jinsi ya kuepuka makosa yanayohatarisha malipo ya madai yao. Aidha, walipongeza maboresho yaliyofanywa katika mifumo, ambayo yamewezesha malipo kufanyika kwa wakati bila ucheleweshaji.

Pia Bw. Luvinga alisisitiza umuhimu wa watoa huduma kutekeleza mafunzo waliyopokea na kutoa huduma kwa uwazi na bila udanganyifu. Aliahidi ushirikiano wa karibu kati ya NHIF na watoa huduma katika kuhakikisha wanachama wanapata huduma bora bila changamoto.

Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa