NHIF ILIVYOTOA HUDUMA BORA MAONESHO YA NANE NANE KITAIFA

NHIF ILIVYOTOA HUDUMA BORA MAONESHO YA NANE NANE KITAIFA Aug 12, 2020

Na Mwandishi wetu,

Sikukuu ya Wakulima huadhimishwa kila mwaka Agosti 8 na kwa mwaka huu yameadhimishwa Kitaifa mkoani Simiyu ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alihitimisha maadhimisho hayo.

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulikuwa ni mmoja wa washiriki wa maonesho hayo ya wakulima kwa lengo kubwa la kuwapa elimu ya umuhimu wa kuwa ndani ya mfumo wa bima ya afya ili waweze kuwa na uhakika wa afya zao na kupata matibabu wakati wowote. Kutokana na utoaji wa huduma bora katika maonesho hayo, Mfuko ulitunukiwa tuzo ya ushindi wa kwanza katika kundi la Mashirika ya Umma.

Mbali na utoaji wa huduma ya elimu, Mfuko pia ulitoa huduma za upimaji wa afya bure kwa wananchi wote waliotembelea banda la Mfuko kwenye maonesho haya na kutoa elimu juu ya kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza. Vipimo vilivyotolewa ni pamoja na vya shinikizo la damu, sukari pamoja na uwiano wa uzito na urefu.

Mwitikio wa wananchi katika banda la Mfuko ulikuwa ni mkubwa ambapo kuanzia tarehe 01.08 hadi tarehe 08.08.2020 jumla ya wananchi 2,089 walihudumiwa kwa elimu na kupima afya zao.

Ili kuhakikisha huduma hizi zinawafikia wananchi wengi zaidi, Mfuko pia ulishiriki katika Maonesho ya Nane Nane katika Kanda zote kwa mikoa ya Morogoro, Dodoma, Mwanza, Arusha, Mbeya, Lindi na Zanzibar. Katika mikoa hii pia huduma hizo zilitolewa na kwa Mikoa ya Dodoma na Mbeya nayo iliibuka washindi katika kundi la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Akizungumza muda mfupi baada ya kutunukiwa tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga alisema kuwa tuzo hiyo imeongeza chachu kwa Watumishi wa Mfuko kuendelea kujituma zaidi katika majukumu yao ya kuwafikia wananchi kila mahali na kuhakikisha wanajiunga na Mfuko ili wawe na uhakika wa matibabu wakati wowote.

Bw. Konga alisema kuwa Mfuko umeshiriki maonesho ya mwaka huu ukijivunia mafanikio makubwa ya kuwa na utaratibu rahisi unaowawezesha wananchi wote kujiunga na huduma za Mfuko.

“Mwaka huu tumefarijika sana kushiriki maonesho haya tukiwa na mafao mbalimbali kwa ajili ya makundi yote kujiunga, tunalo fao kwa ajili ya wakulima kupitia Ushirika Afya ambao wanajiunga kwa gharama ndogo kabisa ya shilingi 76,800 kwa mwaka na

anahudumiwa kwenye zaidi ya vituo 7,000 nchi nzima kwa mwaka, pia kundi la watoto chini ya umri wa miaka 18, wanafunzi, mwananchi mmoja mmoja kupitia mpango wa vifurushi ambao unamwezesha kujiunga kwa kuchagua kulingana na mahitaji yake,” alisema Mkurugenzi Mkuu Bw. Konga.

Aliongeza kuwa Mfuko utaendelea kushiriki maonesho mbalimbali na kuongeza juhudi za kuwafikia wananchi katika maeneo yao ili kuwahamasisha na kuwapa elimu ili wachukue hatua za kujiunga.

“Katika kipindi hiki ambacho nchi iko katika Uchumi wa Kati, suala la afya ni la msingi sana na kipimo kikubwa cha maendeleo ni uhakika wa wananchi kupata huduma za matibabu kwa utaratibu rahisi wa bima ya afya, wananchi wanaweza kushiriki shughuli za maendeleo endapo watakuwa na afya njema hivyo kwa kuwa Mfuko una dhamana hiyo utahakikisha unafanya jitihada za kufanikisha suala hilo,” alisema Bw. Konga.