NHIF KUANZA KAMPENI YA UANDIKISHAJI KIJIJI KWA KIJIJI

NHIF KUANZA KAMPENI YA UANDIKISHAJI KIJIJI KWA KIJIJI Dec 06, 2018

Na Grace Michael, Tandahimba

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umesema unaanza rasmi kampeni ya uandikishaji ya kijiji kwa kijiji katika Mikoa ya Mtwara na Lindi ili kuwawezesha wananchi hao kuwa kwenye utaratibu mzuri wa kupata huduma za matibabu.

Imeelezwa kuwa, wananchi wamekuwa wakiingia katika umasikini mkubwa kwa kulazimika kuuza mali za familia kwa lengo la kupata fedha za kugharamia huduma za matibabu.

Hayo yamesemwa naMkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga wilayani Tandahimba ambaye alikuwa miongoni mwa watendaji walioambatana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu katika ziara yake ya kutembelea vituo vya huduma na uhamasishaji wa wakulima kujiunga na NHIF, kupitia Mpango wa Ushirika Afya.

“Nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri na wananchi wote walioko hapa, timu yangu inaanza rasmi kampeni ya kijiji kwa kijini kuanzia wiki ijayo kwa lengo la kumfikia kila mkulima aliyeko katika Mkoa wa Mtwara na Lindi ili wananchi hawa wawe kwenye mfumo bora wa kupata huduma za matibabu wakati wowote,” alisema Bw. Konga.

Alisema kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wote wako kwenye sekta ya kilimo hususan maeneo ya vijijini na kwa kutambua umuhimu wa kulitunza kiafya kundi hili, Mfuko ulianzisha mpango maalum unaojulikana kwa jina la Ushirika Afya unaowawezesha kujiunga na huduma za NHIF kwa gharama nafuu.

Akizungumzia upatikanaji wa huduma za matibabu, Mhe. Waziri Ummy, alisema kuwa Serikali imetengeneza utaratibu rahisi kwa wananchi wake juu ya upatikanaji wa huduma za uhakika za matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambao una jukumu la kugharamia matibabu kwa wanachama wake.

“Hakuna sababu yoyote kwa sasa ya kushindwa kujiunga na NHIF, Serikali ya Awamu ya Tano imeboresha huduma na upatikanaji wa dawa kwa sasa ni mkubwa ambao unamwezesha kila mgonjwa kupata huduma anazozihitaji hivyo nawaomba wananchi wote mjiunge na NHIF ili muwe na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote hata ambao hamna fedha,” alisema Mhe. Ummy.

Alisema kuwa suala la kulinda afya za wananchi ni suala muhimu kutokana na ukweli kwamba bila ya afya njema ama uhakika wa matibabu hakuna shughuli zozote za maendeleo zinazoweza kufanyika.

Kwa upande wa wananchi wamemhakikishia Mhe. Waziri kuwa wako tayari kujiunga na NHIF na kuunga juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Walitumia nafasi hiyo kumuomba Mhe. Waziri kufikisha salaam zao kwa Mhe. Rais Magufuli kuwa wanaridhishwa na utendaji kazi wake hivyo wako tayari kuhakikisha ndoto zake za kuifanya Tanzania kuwa na Uchumi wa Kati zinafikiwa.

Mwisho.