NHIF na TAHLISO Wakubaliana Bima ya Afya kwa kila Mwanafunzi.

NHIF na TAHLISO Wakubaliana Bima ya Afya kwa kila Mwanafunzi. Sep 14, 2021

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na SHIRIKISHO la Viongozi wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Kati Nchini (TAHLISO) wamejadili na kukubaliana kuendelea kushirikiana kuhakikisha kila mwanafunzi wa chuo kikuu na cha kati anakuwa na kadi ya NHIF kwa uhakika wa matibabu. TAHLISO imepongeza NHIF kutoa ushirikiano mkubwa katika kuwahudumia wananfunzi pale panapokuwepo na uhitaji.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa TAHILISO Bw. Frank Nkinda wakati akizungumza katika mkutano kati ya NHIF na Viongozi wa shirikisho hilo Jijini Dodoma.

“Kwa kweli kabla sijawa kiongozi wa TAHLISO sikua naijua NHIF vema lakini sasa nimeweza kuifahamu na naweza kujibu simu nyingi za wanafunzi ninazopokea wanapopata changamoto lakini naushukuru uongozi wa NHIF unakuwepo kutatua matatizo pale zinapotokea,” alisema Bw. Nkinda
Mbali hayo, amesema wao kama viongozi wa wanafunzi wako mathubuti katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu ya kutosha kuhusu bima ya afya kwa wanafunzi ili kuwa uhakika wa matibabu awapo vyuoni.

“Nahimiza tuwe na mpango mathubuti wa kuhakikisha kuwa maagizo ya Mhe. Waziri Mkuu kuhusu ulazima wa wanafunzi wa vyuo vyote vikuu na vya kati nchini yanatekelezwa kwa vitendo.” alisema Bw. Nkinda.

Alisisitiza kuendelea kwa ushirikiano wa NHIF na viongozi wa wanafunzi katika vyuo hivyo kuendeleza mahusiano mazuri ambayo yamejengwa ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali zinapojitokeza na kuondoa malalamiko ya yasiyokuwa ya msingi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga wakati akifungua mkutano huo, niwakumbushe lengo hasa la Mfuko kuanzisha mpango wa huduma za bima ya afya kwa wanafunzi lilikuwa ni kumwondolea mwanafunzi mzigo wa gharama za matibabu ili aweze kuwa na ujasiri wa kuendelea na masomo yake bila kikwazo cha afya yake akiwa chuoni na wakati wa likizo.

“Naomba niwajulishe kuwa Mfuko uko katika maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake na hatuwezi sahau mchango wa kundi la wanafunzi ambao ni wadau wa Mfuko na kuona njia bora ya kuweza kuendeleza mashirikiano mazuri yaliyopo.

Aliendelea kusema kuwa ufanisi wa utekelezaji wa mpango huu unategemea sana ushirikiano wa pande zote ikiwa ni Wanafunzi wenyewe, Chuo husika na Mfuko huu. Bila ya ushirikiano na kila upande kutekeleza wajibu wake ipasavyo hatuwezi kuepuka changamoto katika utekelezaji na mwathirika mkuu anakuwa mwanafunzi.

Hata hivyo hapo nyuma kulikuwa na changamoto kubwa ya wanafunzi kukosa vitambulisho vya bima ya afya kwa wakati, changamoto ambayo kwa kiasi kikubwa imeshughulikiwa cha msingi ni kuendelea kuwa na ushirikiani kwenye kutekeleza hilo.

Mwisho