NHIF YAHIMIZA ELIMU YA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

NHIF YAHIMIZA ELIMU YA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA Oct 12, 2023

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umewahamasisha wananchi kupima afya zao na kupata elimu ya kuishi mtindo bora wa maisha ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.

Huduma hizo zinatolewa katika banda la NHIF kwenye maadhimisho ya Wiki ya Vijana yanayoendelea mkoani Manyara yatakayoambatana na kilele cha mbio mwishoni mwa wiki hii.


Akizungumzia huduma hizo, Meneja wa NHIF mkoa wa Manyara Bi. Joyce Sumbwe amesema kuwa huduma hizo zinatolewa bure hivyo wananchi wafike kupata elimu na kujua hali za afya zao.

"Huduma hizi ni bure lakini pia mwananchi akifika hapa tunampa pia elimu ya umuhimu wa kuwa na bima ya Afya ili awe na uhakika wa kupata huduma za matibabu endapo ataugua," alisema Bi. Sumbwe.


Vipimo vinavyofanyika bandani hapo ni pamoja na shinikizo la damu, sukari na hali lishe.

Bi. Sumbwe amesema kwamba Mfuko umeweka jitihada kubwa ya kutoa elimu ya kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuwa ni magonjwa yanayomaliza nguvu kazi ya Taifa na yana gharama kubwa katika kuyatibia.

"Niwaombe sana wananchi mtumie fursa hii, unapojua hali ya afya yako itakusaidia kujipanga vyema kimaendeleo na kuepuka kuingia kwenye umasikini unaosababishwa na magonjwa yanayoweza kuepukika," alisema Bi. Sumbwe.