NHIF YAJA NA MAPINDUZI MAKUBWA YA KIHUDUMA

NHIF YAJA NA MAPINDUZI MAKUBWA YA KIHUDUMA Nov 26, 2024


Maboresho Mifumo ya Usajili kumaliza changamoto

Sasa wanafunzi kuanzia Awali hadi Chuo kujiunga kiurahisi

Yaondoa ulazima wa shule kusajili wanafunzi 100

Katika kuanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umefanya mapinduzi makubwa ya kimfumo katika huduma zake ili kuwawezesha watanzania wote kujihudumia na kunufaika na huduma zake.

Maboresho yaliyofanywa na NHIF hususan katika kuongeza kasi ya Usajili wa wanafunzi na watoto wenye umri chini chini ya umri wa miaka 21, Mfuko umeunganisha mfumo wa usajili wa Mfuko na taasisi zinazosimamia sekta ya elimu ikiwemo NECTA, NACTVET na TCU ili kurahisisha zoezi la utambuzi wa wanafunzi na utoaji wa namba za malipo kwa wazazi au shule kutegemeana na chagua la shule au chuo husika.

Akizungumzia maboresho yaliyofanyika katika eneo la Mfumo wa Usajili, Kaimu Mkurugenzi wa Wanachama Bw. Hipoliti Lello, amesema kuwa maboresho hayo yameondoa ulazima wa shule au chuo kusajili wanafunzi 100 au zaidi na badala yake wanafunzi hao watajiunga wote kwa idadi iliyopo.

“Mfumo pia kwa sasa unawawezesha wazazi au walezi kupokea na kulipia namba za malipo moja kwa moja bila kupitia chuoni au shule husika hivyo niwaombe wazazi kutumia fursa hii kujiunga na Mfuko,” alisema Bw. Lello.

Akizungumzia idadi ya wanafunzi wanaonufaika kwa sasa, alisema kuwa hadi kufikia Novemba 26, 2024 jumla ya Wanafunzi 147,953 wa shule za awali, msingi, sekondari na vyuo wenye umri chini ya miaka 21 wananufaika na huduma za Mfuko.

Aidha, Mfuko umeandikisha wategemezi 233,554 wenye umri chini ya miaka 21 kupitia wazazi na walezi wanaonufaika na huduma za Mfuko kupitia Mpango wa Vifurushi, Wafanyakazi wa Sekta Binafsi na Umma

Ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanajiunga, Mfuko unaendelea na kampeni maalum ya uhamasishaji wananchi kujiunga wakiwemo wanafunzi kupitia shule mbalimbali.

Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa