Na Grace Michael, Dodoma
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umepongezwa kwa mapinduzi chanya ya kihuduma ambapo kwa sasa inalipa madai kwa Watoa huduma kwa wakati ikilinganishwa na hapo awali.
Mbali na ulipaji wa madai, maboresho ya mifumo yaliyofanyika yamewezesha utatuaji wa changamoto na mawasiliano ya haraka kati ya Mfuko na Watoa huduma hatua inayorahisisha huduma kwa wanachama.
Hayo yamesemwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Ibenzi Ernest wakati akizungumzia mashirikiano ya NHIF na Hospitali hiyo.
"NHIF kwa sasa inastahili kupongezwa kwa namna ilivyojipanga katika kutoa huduma na kwa upande wetu kama Watoa huduma tunalipwa kwa wakati na inapotokea changamoto tunakaa na kuitatua kwa haraka," amesema Dkt. Ibenzi.
Akizungumzia umuhimu wa Bima ya Afya, Dkt. Ibenzi amewataka wananchi kujiunga na NHIF kwa kuwa ndio mkombozi mkubwa katika suala la uhakika wa matibabu.
"Hakuna namna nyingine kwa sasa zaidi ya kupata huduma kupitia Bima ya Afya, wananchi wanaopata huduma kwa kadi wanakuwa na uhakika zaidi wa kupata huduma zote wanazozihitaji tofauti na wananchi wasikuwa na kadi hivyo niwaombe wananchi wajiunge ili wawe na uhakika wa kupata huduma bila kikwazo cha fedha," amesema Dkt. Ibenzi.
Jengo la Huduma ya mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma
Kwa upande wa huduma Hospitalini hapo, amesema Serikali imewekeza vya kutosha katika maeneo yote hivyo ameweka wazi kuwa kwa sasa wana jukumu la kuwahudumia wananchi kwa utaalam na weledi zaidi.
Kwa upande wa wanachama waliokuwa wakipata huduma, wamesema kwa sasa wanapata huduma zote wanazozihitaji na wameahidi kuulinda Mfuko ili uendelee kuwa imara na uhudumie wananchi wengi zaidi.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa