NHIF YASHEHEREKEA PASAKA KWA KUWAHUDUMIA WANAGEITA

NHIF YASHEHEREKEA PASAKA KWA KUWAHUDUMIA WANAGEITA Apr 04, 2018

Na Grace Michael, Geita

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umesherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa kutoa huduma za upimaji wa Afya bure pamoja na kukabidhi kadi za matibabu kwa watoto chini ya umri wa miaka 18.

Huduma hizo zimetolewa katika viwanja vya Soko la Zamani mkoani Geita ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa Mfuko huo wa kuwahudumia wananchi kwa kuwafikia katika maeneo yao.

Utoaji wa huduma hizo, ulihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Bi. Martha Mkupasi ambaye alipongeza juhudi zinazofanywa na Mfuko za kuhakikisha wananchi wote wananufaika na huduma zake.

“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mliyoifanya hapa, lakini pia kwa wananchi ambao mmejitokeza kufika katika banda hili na kutumia huduma ambazo Serikali yenu imezileta, kama tunavyojua mtaji mkubwa wa mwananchi ni afya yake kwanza hivyo tumieni hii fursa ambayo mfuko imeleta ili kwa pamoja tuweze kufanya shughuli za maendeleo na kuchangia pato la familia na taifa letu,’ alisema Bi. Mkupasi.

Aliwataka wananchi kuhakikisha wanajiunga na huduma za Mfuko kabla ya kuugua ili kujihakikishia huduma za matibabu wakati wowote wanapopata matatizo ya ugonjwa.

Kwa upande wa Serikali, alisema kuwa itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mfuko kwa kuwahamasisha wananchi kujiunga na huduma zake ambazo zinalenga kumuondolea usumbufu mwananchi hasa wakati anapopatwa na magonjwa.

Kwa upande wa Meneja wa Mkoa wa Geita, Dk. Mathias Sweya akitoa takwimu za wananchi walioshiriki zoezi hilo alisema kuwa, jumla ya wananchi 812 wamefika bandani hapo na kupata huduma mbalimbali ikiwemo ya elimu juu ya huduma za NHIF, usajili wa watoto na upimaji wa afya.

“Waliopata huduma ya upimaji wa afya ni 740, ambapo wamebainika na uzito uliokithiri ni asilimia 11.4, shinikizo la damu asilimia 7.8 na Sukari ni asilimia 0.4 huku jumla ya watoto 51 wakisajiliwa na huduma za Mfuko,” alisema Dk. Sweya.

Huduma hizi zimekuwa zikitolewa na Mfuko katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa lengo la kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kwa kutoa elimu ya kujikinga lakini pia kuhamasisha wananchi kujiunga na huduma za mfuko.