RAIS WA CHAMA CHA WAUGUZI NA WAKUNGA AFURAHISHWA NA HUDUMA ZA NHIF, ATAKA USHIRIKIANO ZAIDI

Imewekwa: 12 May, 2025
RAIS WA CHAMA CHA WAUGUZI NA WAKUNGA AFURAHISHWA NA HUDUMA ZA NHIF, ATAKA USHIRIKIANO ZAIDI

Iringa, Mei 11, 2025* 

Rais wa Chama cha Wauguzi na Wakunga Tanzania (TANNA), Bw. Alexander Baluhya, ameonesha kuridhishwa kwake na huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya TANNA na NHIF ili kufanikisha lengo la serikali la kufikia bima ya afya kwa wote.

Akizungumza alipotembelea banda la NHIF katika maonyesho ya Mkutano Mkuu wa TANNA unaoendelea Mkoani Iringa, Bw. Baluhya alisema kuwa wauguzi na wakunga ndio wanaohudumia jamii kwa ukaribu mkubwa, hivyo wana nafasi nzuri ya kuhamasisha wananchi wengi zaidi kujiunga na NHIF.

“Huduma za NHIF zimeendelea kuboreshwa kwa kiwango kikubwa, na kama chama, tunafurahishwa na juhudi hizo. Ushirikiano kati ya NHIF na TANNA utasaidia sana katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa bima ya afya, kwa kuwa sisi tunakuwa nao kila siku,” alisema Bw. Baluhya.

Aidha, aliongeza kuwa NHIF ni mfuko mkubwa wenye uwezo mkubwa wa kuwahudumia Watanzania wengi, na hivyo ni muhimu kuwahusisha wadau wote wa sekta ya afya katika kutekeleza mpango wa serikali wa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya kupitia bima.

“Ushirikiano huu si tu unaleta tija kwa mfuko na wanachama, bali unaiwezesha serikali kufikia kwa haraka malengo yake ya kuwa na jamii yenye afya bora na iliyoandaliwa vyema kwa maendeleo ya taifa,” aliongeza.

Mkutano huo mkuu unawakutanisha wauguzi na wakunga kutoka mikoa yote ya Tanzania kwa lengo la kujadili changamoto na mafanikio katika sekta ya afya, huku taasisi mbalimbali, zikiwemo NHIF, zikitumia jukwaa hilo kuonesha huduma na fursa wanazotoa kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.