SERIKALI imeihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Afya na Masuala ya UKIMWI, kuwa suala la huduma za matibabu kwa wasiokuwa na uwezo limezingatiwa na fedha zimeanza kuwekwa kwenye Mfuko wa kuhudumia kundi hilo.
Akiwasilisha taarifa ya maandalizi ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama, amesema hatua iliyofikiwa ni kuunganisha mifumo ya TASAF na mifumo ya usajili wa wanachama ya NHIF kupitia mradi wa maboresho ya Mifumo ya TEHAMA.
Alisema katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali imebainisha vyanzo mahsusi vya kugharamia kundi hilo la wananchi vinavyokadiriwa kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 173.5,” alisema Mhe. Mhagama.
“Katika suala hili la Bima ya Afya kwa Wote, tumejipanga vizuri kuhakikisha wananchi wanahamasika kujiunga ili waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika eneo la huduma za matibabu. Kwa upande wa wasiokuwa na uwezo, Serikali imelizingatia hili na imeanza kuweka fedha katika Mfuko wake,” alisema Mhe. Mhagama.
“Kifungu cha 25 cha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Sura namba 161 kimeanzisha Mfuko wa kugharamia Bima ya Afya kwa watu wasio na uwezo, ambapo Serikali imejipanga kuanza ugharamiaji wa Bima ya Afya kwa wote kwa kaya Milioni 1.2 ambazo zinatambuliwa kama kaya zenye umaskini uliokithiri,” amesema Waziri Mhagama.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kushirikisha wadau mbalimbali ikijumuisha watoa huduma za afya na wadau wa maendeleo katika Sekta ya Afya ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa wote unatekelezeka kwa ufanisi mkubwa, hivyo wananchi ambao hawana uwezo watanufaika na huduma hizo.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Elibariki Kingu alipongeza hatua hiyo iliyofikiwa na kusisitiza matumizi ya Mifumo katika huduma ili iweze kutatua changamoto za masuala ya udanganyifu na kuondoa uwezekano wa vipimo au dawa kutolewa zaidi ya mara moja kwa siku husika.
“Mifumo ndio njia pekee itakayosaidia kuokoa fedha nyingi na kuondoa changamoto za udanganyifu, Mifumo ya hospitali isomane ili kuweza kubadilishana taarifa za wagonjwa nah ii itasaidia kuokoa fedha nyingi kwa kuepuka kufanya vipimo vilivyofanywa na hospitali nyingine hivyo tuhakikishe mifumo iko vizuri,” alisisitiza Mhe. Kingu.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka, alielezea maboresho yaliyofanyika kwenye upande wa Mifumo ni pamoja na Mifumo ya NHIF kusomana na Mifumo ya hospitali mbalimbali na taasisi ikiwemo RITA, WCF, NACTE, NSSF, NIDA, BRELA, Wizara ya Afya, Wizara ya Fedha na zingine zinazoshirikiana na Mfuko katika utoaji wa huduma ili kurahisisha utambuzi wa mwanachama husika na nyaraka zinazohitajika.
Mwisho