Watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na kwa kujituma zaidi ili kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwahudumia wananchi wengi zaidi kupitia mfumo wa bima ya afya.
Agizo hilo limetolewa leo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Bw. Juma Muhimbi wakati akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Mfuko huo ambalo limeketi kisheria na kwa lengo la kuweka mikakati ya uboreshaji wa huduma kwa wanachama wake.
“Kama mnavyofahamu azma ya Serikali yetu inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwafikia wananchi wote ili waweze kupata huduma za matibabu kupitia bima ya afya, hivyo katika hili niwaombe sana muweke nguvu na kutumia mbinu mbalimbali za elimu na uhamasishaji ili wananchi waweze kujiunga,” alisema Bw. Muhimbi.
Akizungumzia kupitishwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, aliwataka watumishi kuwa tayari kuwahudumia wananchi wengi zaidi na kurahisisha huduma kwa kutumia mifumo ya TEHAMA. Aidha, aliwataka kuweka mikakati ya kuwafikia wananchi mpaka vijijini kwa kuwapa elimu ya manufaa makubwa yaliyomo ndani ya sheria na kuwahamasisha kujiunga ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu.
“Maandalizi ya utekelezaji wa sheria na mikakati mnayoweka ndio inatoa taswira au mwanga wa mafanikio katika hili na tukumbuke kuwa suala la wananchi kupata huduma bora ndio matamanio ya Rais wetu lakini pia ndio dhamana ambayo tumepewa sisi kwa ajili ya wananchi wa Tanzania.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw. Bernard Konga alisema kuwa tayari mikakati mbalimbali imewekwa kwa ajili ya kuwafikia wananchi kwa kuwapa elimu na kuwahamasisha lakini pia maandalizi yamefanyika kupitia mifumo ili kuwezesha utoaji wa huduma bora.