Na Mwandishi Wetu, Mbeya
SERIKALI mkoani Mbeya imesema itachukua hatua kali kwa mtu yeyote atakayejihusisha na udanganyifu wa huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Onyo hilolimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Albert Chalamila wakati akifungua mkutano wa wadau wa NHIF mkoani humo. “Kufanya udanganyifu kwa huduma za Mfuko ni kuhujumu jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali za kumairisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi, hivyo ndani ya Mkoa huu sitavumilia kuona hili.
“Tunasikia kuna baadhi ya wadau wa Mfuko wasio waaminifu wamekuwa wakihujumu Mfuko huu, kwa upande wa Mkoa wa Mbeya niliweke tu wazi kuwa atakayejihusisha na udanganyifu wowote nitakula naye sahani moja, ni lazima huu Mfuko tuulinde ili uweze kuhudumia wananchi na hata vizazi vijavyo,” alisema Bw. Chalamila.
Ili kuhakikisha huduma za Mfuko zinalindwa, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wadau wote mkoani humo kuhakikisha kila mmoja anakuwa mlinzi wa huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Akisisitiza juu ya wananchi kujiunga na huduma za Mfuko, ameweka wazi kuwa ili taifa liweze kufikia malengo yake na kutimiza ndoto ya Rais Dkt. John Magufuli ya Tanzania kuwa ni nchi ya Uchumi wa Kati kupitia uwekezaji wa Viwanda ni lazima huduma za matibabu ziwe za uhakika kwa wananchi wote.
“Ni azma ya Serikali hii kuwafikia watanzania wote na huduma bora za matibabu kupitia Bima ya Afya, kukamilika kwa azma hii kutaruhusu watu wengi zaidi kutumia huduma za matibabu ambazo awali walishindwa hivyo niwaombe tu watoa huduma mjipange kuweka mazingira mazuri ya kuwahudumia watu hawa,” alisema Mkuu wa Mkoa.
Alisema kuwa kwa sasa Serikali imeimarisha upatikanaji wa dawa katika hospitali zote za Serikali hatua ambayo imeondoa malalamiko ya awali ya ukosefu wa huduma bora hususan dawa hivyo ni wakati wa wananchi kujiunga na NHIF ili wawe na uhakika wa huduma za matibabu wakati wowote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF, Mama Anne Makinda amewataka watoa huduma kuhakikisha wanashirikiana na Mfuko katika kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa mwanachama ni bora zaidi kutokana na ukweli kwamba wanachama hao wamelipia huduma kabla ya kuugua.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Mfuko, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko, Bwana Bernard Konga amesema kuwa maboresho mbalimbali yamefanyika ndani ya Mfuko kuhakikisha huduma zinakuwa bora zaidi.
Amesema kuwa kwa sasa Mfuko unawalipa watoa huduma madai yao kwa wakati ili kuepukana na changamoto za kukwamisha huduma kwa wanachama hivyo akatumia nafasi hiyo kuwaomba Watoa huduma kuhakikisha nao kwa upande wao wanatoa huduma bora na kuwapa wanachama ujumbe ulio sahihi.
“Wapo baadhi ya watoa huduma ambao mwanachama wetu akifika anataka huduma fulani anamwambia huduma hii hailipiwi na Mfuko au Mfuko umechelewesha madai kumbe huduma hiyo haistahili kutolewa kituoni hapo kulingana na ngazi ya kituo chake hivyo ni vyema mkawapatia wanachama wetu taarifa zilizo sahihi,” alisema Bw. Konga.
Amewataka wanachama kuendelea kutoa maoni yao ya kuboresha huduma kupitia njia mbalimbali zilizowekwa na Mfuko ikiwemo kituo cha Huduma kwa Wateja, Kusara za Mfuko za Mitandao ya Kijamii, mikutano ya wadau na njia zingine ili kuendelea kuimarisha zaidi huduma za Mfuko.
Akizungumzia namna Mfuko ulivyojipanga kupambana na udanganyifu amesema kuwa, Mfuko umeimarisha Mifumo yake ya TEHAMA na kuanzisha kitengo maalum ambacho kinapambana na udanganyifu ambao unafanywa na baadhi ya wanachama na watoa huduma, hivyo akawaomba wadau wote na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kila mmoja analinda uhai wa Mfuko ambao kwa sasa unahudumia asilimia 32 ya Watanzania wote.
Mwisho.