SUALA LA BIMA YA AFYA SIO LA KUBISHANA- SHIGELLA

SUALA LA BIMA YA AFYA SIO LA KUBISHANA- SHIGELLA Mar 19, 2020

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigella amesema kuwa jambo linalohusu kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya jambo la kubishana bali ni la kutekeleza kwa kuwa afya ndio msingi wa maendeleo na unapokuwa na uhakika wa matibabu unakuwa na amani.

Hayo aliyasema wakati wa uzinduzi wa mpango wa uhamasishaji wa wananchi kujiunga na vifurushi vya Bima ya Afya mkoani humo Januari 18, mwaka huu.

“Kumekuwa na mazoea Fulani au utaratibu wa watanzania wengi kuona afya ni suala la mchezo, hatupendi kuchukua tahadhari juu ya afya zetu wakati, umefika wakati wa kila mtanzania kuona afya ni nyenzo kubwa katika kujiletea maendeleo maana bila ya afya njema huwezo kufanya jambo lolote la kijamii ama la kimaendeleo,”-Alisema Mhe. Shigella.

Aidha Mhe. Shigella aliongeza kuwa mpango wa vifurushi vya Bima ya Afya ni Mkombozi katika sekta ya afya, hivyo watanzania watumie fursa hiyo ili waweze kufaidi maboresho makubwa yanayaoendelea kutekelezwa na Serikali ya awamu ya tano katika sekta ya afya.

Kutokana na umuhimu huo, Mhe. Shigella aliagiza viongozi wote mkoani huo kuhakikisha wanalibeba suala la uhamasishaji kwa wananchi katika maeneo yote ya Mkoa wa Tanga ili wananchi wafahamu umuhimu wake na hatimaye wachukue hatua za kujiunga.

Akizungumza katika Uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Bima ya afya Mama. Anne Makinda amewataka watanzania kujiunga na mpango wa Bima ya Afya ambao ndio mfumo bora wa afya duniani kote.

“Popote unapoenda duniani suala la Bima ya ni muhimu sana, Bima ya afya ndio mkombozi, Bima ya afya ndio maisha itakayokusaidia popote pale na muda wowote hata kama ukiwa huna pesa, vifurushi hivi vitakuwezesha kupata matibabu popote pale duniani”-Mama. Makinda.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga aliwahakikishia wananchi wa Mkoa wa Tanga kuwa watakapojiunga na NHIF hawatajutia uamuzi huo kutokana na namna huduma zilizovyoboreshwa kwa wanachama wa Mfuko.

“Tumeanzisha mpango huu lakini jambo kubwa ambalo tumejipanga ni katika kuwahudumia wanachama wetu, tunao mtandao mkubwa sana wa vituo vya kutolea huduma za matibabu hivyo kwa wananchi watakaojiunga na NHIF hawatajutia huduma,” alisema Bw. Konga.