TEKELEZENI AGIZO BILA KUSUMBUA WANACHAMA WA NHIF- RMO Arusha

TEKELEZENI AGIZO BILA KUSUMBUA WANACHAMA WA NHIF- RMO Arusha Jun 01, 2022

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt. Sylvia Mamkwe ameviagiza Vituo vyote vya kutolea huduma za matibabu kwa Wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoani Arusha, kutowasumbua wanachama hao wakati wa utekelezaji wa agizo la kutotoa fomu za kuchukuliwa dawa katika maduka ya dawa nje ya kituo.

Agizo hilo amelitoa mbele ya Watoa Huduma wa Mkoa wa Arusha wakati wa kujadili utekelezaji wa agizo la Serikali la kutotoa fomu 2C ambayo humwezesha mwanachama kupata dawa nje ya kituo husika.
"Tutekeleze hili bila kuwapa usumbufu wowote wanachama, mwanachana anapofika kituoni anachohitaji ni kupata huduma zote hivyo tuhakikishe hawakosi huduma na haiwaathiri kwa namna yoyote" ameagiza.

Aidha amevitaka vituo vyote vya Serikali kuboresha na kuimarisha maduka yao ya dawa ya ndani ya hospitali kama suluhu ya kupata dawa kituoni.

"Nia kubwa ya Serikali katika hili ni kuboresha huduma kwa wanachama na wananchi kwa ujumla na kuzuia vitendo vya udanganyifu hivyo wote tunapaswa kutekeleza hili," alisisitiza.

Naye Meneja wa NHIF Mkoa wa Arusha Bw. Isaya Shekifu amewahakikishia Watoa huduma wote ushirikiano wa kutosha katika kipindi hiki ili kuwezesha upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama.

Mwisho.