TUCTA YAIPONGEZA NHIF KUTEKELEZA AGIZO LA UMRI WA WATEGEMEZI

TUCTA YAIPONGEZA NHIF KUTEKELEZA AGIZO LA UMRI WA WATEGEMEZI Sep 13, 2021

SHIRIKISHO la Vyama Vya Wafanyakazi (TUCTA) limeupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Hassan Suluhu ya kuongeza umri wa watoto wategemezi wa wanachama wa Mfuko huo kutoka miaka 18 hadi miaka 21.
Pongezi hizo zimetolewa na Rais wa TUCTA, Bw. Tumaini Nyamhokya wakati akizungumza katika mkutano kati ya NHIF na Viongozi wa vyama vya wafanyakazi leo Jijini Dodoma.
“Kwa kweli tuna kila sababu ya kuwapongeza, kuna mambo sasa yanaonekana kwa macho, hakuna asiyeona huduma zinazopatikana kwa wanachama wa NHIF lakini kubwa zaidi niwapongeze sana kwa utekelezaji wa agizo la Rais ambalo sisi kama wawakilishi wa Wafanyakazi tulimuomba na akaagiza kwenu mlitekeleze,” alisema Bw. Nyamhokya.
Mbali na pongezi hizo, ameshauri pia Mfuko kuhakikisha unapanua wigo wa huduma zake kwa kuwafikia wananchi wengi zaidi hususan wa maeneo ya vijijini ili kila mtanzania awe na uhakika wa matibabu bora na ya uhakika.
“Bima ya afya ni ya muhimu sana kwa kila mwananchi, binafsi ni shahidi mwaka juzi hadi mwaka jana niliugua na nilitumia fedha nyingi zaidi ya shilingi milioni 15 ambazo ni nje ya gharama za usafiri na mambo mengine hivyo nisingekuwa na bima ya afya ina maana fedha zote hizo zingetoka ndani ya familia, hivyo tuendelee kuwafikia wananchi wote,” alishauri Bw. Nyamhokya.

Akizungumzia ushirikiano wa NHIF na vyama vya wafanyakazi, aliutaka Mfuko kuendeleza mahusiano mazuri ambayo umejenga kwa vyama hivyo ili kuwezesha utatuzi wa pamoja wa changamoto mbalimbali zinapojitokeza na kuondoa malalamiko ya wafanyakazi yasiyokuwa ya msingi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga wakati akifungua mkutano huo, alisema kuwa Mfuko unatambua mchango mkubwa wa vyama vya wafanyakazi katika utoaji wake wa huduma na maboresho mbalimbali ambayo yanafanywa na Mfuko hivyo akaahidi kuendeleza uhusiano huo.
“Wakati tunaadhimisha miaka 20 ya Mfuko, hatuwezi kusahau kutambua mchango wa vyama vya wafanyakazi katika safari hii. Pamoja na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza, lengi ni kuboresha huduma zetu hususan kwa kundi la wafanyakazi hivyo ni lazima tuendeleze mashirkiano haya,” alisema Bw. Konga.

Kwa sasa Mfuko uko katika maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, umetoka mbali kiutekelezaji wa majukumu yake na umeendelea kushirikiana na wadau wake katika kutekeleza haya. Akiongelea Mfuko ulipotoka na ulipo na mafanikio ambayo yamefikiwa kwa kipindi cha miaka 20, amesema kwa sasa wananchi wote wamewekewa utaratibu wa kujiunga na Mfuko tofauti na hapo awali ambapo makundi machache na hasa watumishi ndio waliwezeshwa kujiunga.

“Mafanikio mengine ni eneo la malipo kwa Watoa huduma ambapo kwa sasa yanalipwa ndani ya muda mfupi kati ya siku 30 hadi 45 ikilinganishwa na awali ambapo ilikuwa ni siku 60 na wakati mwingine kuzidi na kufikia 100 na malipo hayo yamewezesha vituo kuwa na mapato ya uhakika ambayo yanawezesha vituo kuimarisha huduma zake,” alisema.

Mfuko pia umefanikiwa kuboresha kitita cha mafao kwa wanachama ambapo kwa sasa huduma ni nyingi zaidi zikiwemo za kitalaam na ambazo awali hazikupatikana hapa nchini. Wigo wa upatikanaji wa huduma kwa wanachama ni zaidi ya vituo 8500 katika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar.
Mwisho.