TUNAWAFIKIA WANANCHI WALIPO - NHIF

TUNAWAFIKIA WANANCHI WALIPO - NHIF Oct 27, 2023

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeendelea na jitihada zake za kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima ya afya na kuhamasisha wananchi kukata bima. Moja ya njia zinazotumika ni kuwafikia wananchi maeneo waliyopo na kuwapa elimu hiyo pamoja na kuwasajili.

Haya yamebainika wiki hii ambapo watumishi wa Ofisi ya NHIF Gongolamboto walisambaa katika maeneo ya mikusanyiko ya wananchi kama masoko, nyumba kwa nyumba, vituo vya daladala, maduka na maeneo mengine ili kuelimisha wananchi.

Akizungumza na wananchi wakati wa uhamasishaji, Msimamizi wa Ofisi ya NHIF Gongolamboto Bw. Cannon Luvinga aliewaelezea wananchi umuhimu wa kuwa na bima ya afya na kuwahimiza wajiunge ili wawe na uhakika wa huduma za matibabu wakati wawote na popote walipo nchini.

Kwa upande wa wananchi, waliupongeza Mfuko kwa kusogeza huduma karibu nao hatua inayohamasisha zaidi kujiunga na kuwa karibu na Mfuko.

"Tunashukuru sana kusogezewa huduma hii ni hatua kubwa itakayotuhamasisha wananchi wengi kujiunga na Mfuko," alisema Bi. Nasra Ally Bakari.

Pamoja na jitihadq hizo, Mfuko umeendelea kufungua ofisi katika maeneo ya kimkakati karibu na wananchi kwa lengo la kuongeza ushawishi kwa wananchi kujiunga.

Ofisi ambazo tayari zimefunguliwa ni pamoja na Gongolamboto, Kigamboni na Ubungo katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mfuko unaendelea na mikakati yake ya kusogeza huduma kwa wananchi ambapo maeneo mengine pendekezwa ni pamoja na Tunduma na Kahama.