Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bw. Bernard Konga akielezea mwelekeo wa utoaji huduma kwa wanachama wa Mfuko wakati alipokutana na Watoa huduma wa Mkoa wa Kinondoni leo.
Baadhi ya Watoa Huduma wa Mkoa wa Kinondoni katika kikao cha pamoja na Uongozi wa NHIF ambao ulijadili namna bora ya utoaji wa huduma za matibabu kwa wanachama wake.
Watoa Huduma wakifuatilia kwa makini majadiliano juu ya uimarishaji wa huduma za matibabu kwa wanachama wa NHIF
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Berard Konga (Kati kati) akisistiza jambo, kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Wanachama, Mbaruku Magawa na Kulia ni Meneja wa Mkoa wa Kinondoni, Innocent Mauki.
Wanachama wakifuatilia mjadala.
TUPAMBANENI NA UDANGANYIFU WA HUDUMA- MKURUGENZI MKUU
Na Grace Michael
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bw. Bernard Konga amewataka Watoa Huduma wote nchini kushirkiana na Mfuko katika kupambana na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wanachama katika kujipatia huduma za matibabu.
Aliyasema hayo leo wakati akizungumza na Watoa Huduma wa Mkoa wa Kinondoni, Dar es Salaam juu ya uimarishaji wa huduma za matibabu kwa wanachama wake hasa katika kipindi hiki ambapo wananchi wengi zaidi wanajiunga na Mfuko huo.
“Niwahimize kwamba kwa pamoja tuunganishe nguvu zetu katika kuulinda huu Mfuko kwa kupambana na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wananchi kwa kushirikiana na baadhi ya wanachama. Uhai wa Mfuko huu unatakiwa kulindwa kwa gharama zozote ili uendelee kuwahudumia Watanzania na uwepo hata kwa vizazi vinavyokuja,” alisema Bw. Konga.
Amewapongeza watoa huduma ambao wamekuwa wakitoa taarifa za udanganyifu walizozibaini katika vituo vyao na kuwaomba waendelee na utaratibu huo ili kuulinda Mfuko. Alisema hatua hiyo inaonesha uzalendo wa Watoa huduma hao katika kuhakikisha Mfuko huo unaendelea na uhai wake kwa manufaa ya wanachama na wananchi kwa ujumla.
“Tumeamua sisi kama NHIF kukutana na watoa huduma wetu wote, tukae na tujadili kwa pamoja ili changamoto zinazotuhusu sisi na nyie watoa huduma tuzimalize ili wanachama wetu wanapofika huko wapate huduma stahiki,” alisema Bw. Konga.
Kwa upande wa Watoa huduma, wameupongeza Mfuko kwa hatua hiyo ya kuendeleza mpango wa kukutana na watoa huduma kwa mazungumzo ya namna bora ya kuimarisha huduma hivyo kwa pamoja wamekubaliana kuendelea kushirikiana na Mfuko kwa karibu ili kuhakikisha huduma bora kulingana na miongozo inawafikia wanachama ikiwa ni pamoja na kuulinda Mfuko huo.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, amewaomba wananchi kutumia fursa iliyopo ya kujiunga na Mfuko ili kuepukana na kujiingiza katika udanganyifu ambao unahujumu Mfuko ambazo zitawapelekea kuingia katika mikono ya sharia.