Katika kuelekea utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, Serikali imekusudia kuwafikia wananchi wote ili wawe kwenye mfumo wa Bima ya Afya unaowezesha kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha.
Akizungumza kwenye mkutano leo uliowajumuisha Watoa huduma nchini, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Wizara ya Afya, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Tumaini Nagu amesema uamuzi wa kuanzisha sheria ya bima ya afya kwa wote ni sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millennia ya kuhakikisha kuwa watu wote wanakuwa na uhakika kwa matibabu.
“Sote tunatambua kuwa Mhe. Rais ameweka kipaumbele kwenye masuala ya afya haswa kwenye ujenzi na uboreshaji wa miundombinu katika ngazi zote za vituo vya kutolea huduma hivyo ni lazima wananchi wetu wajiunge na bima ya afya ili waweze kufaidi au kunufaika na huduma hizi zilizoboreshwa,” alisema Dkt. Nagu.
Amesisitiza kuwa ili kuwezesha uwepo wa utaratibu mzuri wa utoaji wa huduma bora ni lazima kila mtu awe sehemu ya uchangiaji wa huduma za afya.
“Tunataka kila mmoja awe na bima hii na sio wale ambao ni wagonjwa tu. Kupata matibabu kwa kutumia utaratibu wa fedha za mfukoni hauna uhakika wa matibabu.” Alisema Dkt. Nagu.
Kutokana na hayo, aliwataka washiriki wa kikao hicho kujadiliana kwa uwazi na kuwasilisha maoni yenye kuwaangalia wananchi wa hali zote kupata bima ya afya.