WAKULIMA WA ZAO LA MKONGE SASA KUNUFAIKA NA HUDUMA ZA BIMA YA AFYA YA NHIF

WAKULIMA WA ZAO LA MKONGE SASA KUNUFAIKA NA HUDUMA ZA BIMA YA AFYA YA NHIF Jul 14, 2021

Na mwandishi.

NHIF na CRDB waliingia makubaliano mnamo tar 5/5/2021 ikiwa ni mwanzo wa ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili katika kuwahudumia wakulima na Bima ya Afya ya NHIF kupitia Vyama vyao vya Msingi vya Ushirika.

Katika tukio hilo, NHIF na Benki ya CRDB wameingia makubaliano na Vyama Vya Msingi vya NGOMBEZI AMCOS, HALE AMCOS, MWELYA AMCOS, MAGUNGA AMCOS na MAGOMA AMCOS vilivyopo Mkoani Tanga.

Mgeni Rasmi katika tukio hili , Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Adam Kigoma Malima amesisitiza vyama vya ushirika kuwa makini na kufanya upembuzi yakinifu ili kujua faida inayotokana na uzalishaji wao na kuweza kupata fursa za mikopo kama hii ha Bima ya Afya ili kuboresha maisha ya kila mwana ushirika.

Aidha Mhe. Malima amewataka Benki ya CRDB kuwa tayari kuwawezesha wakulima kwa kuwapatia mikopo ya uzalishaji ili waweze kuzalisha kwa faida zaidi na kuweza kjiunga na huduma ya Bima ya Afya.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uanachama Ndugu Hipolit Lelo alielezea namna wakulima wanavyonufaika na huduma za Bima ya Afya na kupata huduma za matibabu hadi hospitali za ngazi zote.

Na kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Biashara wa CRDB Ndugu Boma Raballa alisema CRDB ina ushirikiano na Bima ya Afya ili kuhakikisha kuwa Afya ya wana Ushirika inaimarishwa zaidi. Alisema CRDB na NHIF tumeanzisha utaratibu huu mzuri wa kuwezesha wakulima kujiunga na Bima ya Afya ili kuwa na Afya Bora.

Naye Meneja wa Ofisi ya NHIF Mkoa wa Tanga Ndugu Ally Mwakababu alisema Huduma hii ya Bima ya Afya ya NHIF itamwezesha mkulima kupata huduma bora za matibabu kwa muda wa mwaka mzima bila kuwa na wasiwasi. Alisema huduma hizo ni kama kumuona daktari, vipimo, kupata dawa, upasuaji mkubwa na mdogo, kulazwa na huduma zote za msingi zilizo katika Kitita cha NHIF. Alisema wanachama wa NHIF wanapata huduma katika vituo zaidi ya 9000 kwa ajili ha kuongeza fursa kwa wanachama wa NHIF kupata huduma za Matibabu.

Mpango huu umeonesha matumaini kwa wana ushirika ikiwa ni siku chache baada ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kuwataka NHIF kuendelea kutoa elimu juu ya huduma hii ya Bima ya Afya ili kumfikia kila mwana ushirika.


#Miaka20yaNHIF Uhakika wa Matibabu kwa Wote .