WANANCHI WATAKIWA KUJIUNGA NHIF KABLA YA KUUGUA

WANANCHI WATAKIWA KUJIUNGA NHIF KABLA YA KUUGUA May 31, 2023

SERIKALI imetoa rai kwa wananchi kujiunga na familia zao kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kabla ya kuugua ili waweze kunufaika na huduma za matibabu bila kikwazo chochote.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akisoma hotuba ya Bajeti ya Mwaka 2023/2024 ambapo amesisitiza kuwa utamaduni uliojengeka wa wananchi kujiunga na NHIF baada ya kuugua ni kinyume na dhana ya bima ya afya.

Amesema kuwa ili kuendelea kuimarisha uhai na uendelevu wa Mfuko, Serikali kupitia NHIF imefanya tathmini ya wanufaika wa huduma zitolewazo kwa kundi la watoto walio chini ya miaka 18, ambao hupata huduma kupitia Mpango ujulikanao kama Toto Afya Kadi.

Alisema mpango huo ulianzishwa mwaka 2016 ukiwa na lengo la kusajili angalau asilimia 10 ya watoto milioni 25 waliokuwepo kwa kuzingatia sensa ya watu ya mwaka 2012 lakini hadi kufikia mwaka 2020/21, Mfuko ulikuwa umesajili watoto 205,796 ambao michango yao ilikuwa ni shilingi bilioni 5.99 na matumizi yao ni shilingi bilioni 40.58.

“Kulingana na tathmini hiyo, kundi hili limekuwa likipata huduma zaidi katika vituo vya ngazi za juu vinavyomilikiwa na Sekta Binafsi ambavyo vililipwa asilimia 58 ya fedha hizo ikilinganishwa na asilimia 22 iliyolipwa kwa vituo vya Mashirika ya Dini na asilimia 20 kwa vituo vya Serikali, kwa magonjwa kama malaria, kikohozi na homa, ambayo yangeweza kutibiwa katika vituo vya ngazi ya chini” alisema Mhe. Ummy.

Kutokana na tathmini hiyo ni wazi kuwa kundi hilo lina matumizi makubwa na hivyo kutishia uhai na uendelevu wa Mfuko endapo hatua hazitachukuliwa hivyo kuanzia mwezi Februari 2023, utaratibu wa kuandikisha kundi hili kwa mtoto mmoja mmoja umesitishwa.

"Msisitizo kwa sasa upo katika usajili kupitia Vifurushi ambavyo vina utaratibu wa kusajili katika ngazi ya familia. Vifurushi hivi vijulikanavyo kama Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya vinatoa fursa kwa familia kusajiliwa kulingana na ukubwa wake pamoja na kipato na kwa watoto wengine wanaweza kusajiliwa kupitia shule wanazosoma, lengo ikiwa ni kusajili watoto wengi kwa umoja wao kulingana na misingi na dhana ya bima ya afya.