Na Grace Michael, Dodoma
WATANZANIA wametakiwa kujenga utamaduni wa kuwa na bima ya afya kabla ya kuugua ili kuepukana na usumbufu wa kutafuta au kutumia gharama kubwa za matibabu wakati wanapopatwa na magonjwa.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima (NHIF), Anne Makinda wakati akizungumza na wadau kutoka Wizara zote Jijini Dodoma.
Amesema kuwa mwananchi anapokuwa na bima ya afya anakuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote bila kujali kama ana fedha ama hana ikilinganishwa na mwananchi ambaye hana bima ya afya ambapo akiugua ni lazima aanze kutafuta fedha za kujitibia.
“Ni lazima ifike mahali watanzania tujenge utamaduni wa kuwa na bima ya afya kabla ya kuugua, tunashuhudia namna wananchi wanavyopata shida wakati wakiwa wamefikwa na maradhi hali inayosababisha wengine hata kulazimisha kutumia njia za mkato au udanganyifu hivyo ili kuepukana na matatizo haya ni vyema tukawa na huu utamaduni wa kukata bima ya afya mapema,”alisema Mama Makinda.
Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli imewekeza fedha nyingi katika sekta ya afya kwa kuhakikisha dawa, vifaa tiba na mahitaji yote katika vituo vya kutolea huduma vinakuwepo ili mwananchi apate huduma kamilifu.
Kutokana na hayo, aliwataka wadau hao kushirikiana na Mfuko kwa karibu kwa kutoa maoni ama ushauri wao kwa uwazi ili kuleta mabadiliko chanya ya kihuduma kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya hasa katika kipindi hiki cha kuelekea afya bora kwa wote.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema, Mfuko umejipanga katika uboreshaji wa huduma zake ikiwemo taratibu zinazowawezesha wananchi kujiunga na huduma zake.
Alisema kuwa, kwa sasa mfuko unaangalia uwezekano wa kumwezesha mwananchi mmoja mmoja kujiunga na mfuko lakini pia utaratibu wa kulipa fedha kidogo kidogo, taratibu ambao zitawawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na huduma za mfuko.
“Tumejipanga na tumedhamiria kufikia mwaka 2020 ni lazima tuhudumie wananchi wengi zaidi na kwa sasa tunajipanga kuzindua huduma mbalimbali ambazo zinalenga kumnufaisha mwananchi wa kawaida kabisa,”alisema.
Akizungumzia suala la huduma bora, alisema mfuko umeweka mazingira rafiki kwa watoa huduma kupata mikopo rahisi kwa ajili ya uboreshaji wa huduma zao hususan vifaa tiba na uimarishaji wa miundombinu hatua ambayo imewezesha upatikanaji wa huduma nyingi na bora kupatikana nchini.
Alitumia mwanya huo pia kukemea tabia ya baadhi ya watoa huduma na wanachama wasio waaminifu ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya udanganyifu ambapo alisema Mfuko hauko tayari kuona vitendo hivyo vikiendelea na badala yake hatua kali zitachukuliwa kwa wanaofanya vitendo hivyo.
Kwa upande wa wadau ambao ni Maofisa Waandamizi kutoka wizara zote, waliupongeza mfuko kwa kazi kubwa ambayo umefanya ya utoaji wa huduma na uwekezaji katika sekta ya afya ambao umesaidia huduma nyingi za kitaalam ambazo awali hazikupatikana nchini kupatikana.